Mdee: Hatuondoki Chadema ‘tunamheshimu Mbowe’
Halima Mdee, Mgombea Ubunge wa Kawe kwa tiketi ya Chadema
ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Halima James Mdee amesema, yeye pamoja na wenzake 18 hawatoondoka ndani ya chama hicho na wanaendelea na utaratibu wa kukata rufaa kupingwa kufukuzwa. Anaripoti Hamis Mguta, Dar es Salaam … (endelea).
Mdee amesema hayo leo Jumanne tarehe 1 Desemba 2020 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kutoa msimamo wao baada ya kufukuzwa uanachama wa Chadema.
Mdee na wenzake 18 walituhumiwa kwa “usaliti, kughushi na uasi” wa chama hicho kwa kujipeleka kuapishwa tarehe 24 Novemba 2020 na Spika Job Ndugai kuwa wabunge wa viti maalum, wakijua chama hicho, hakijapendekeza majina yao Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Uamuzi wa kamati kuu, ulitolewa mbele ya waandishi wa habari na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe tarehe 27 Novemba 2020 akisema, Mdee na wenzake wamekisaliti chama na kama hawaridhiki na uamuzi huo, wanaweza kukata rufaa baraza kuu ndani ya siku 30 au kuomba radhi.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari amesema, “mimi na wenzangu, tutakuwa wana Chadema king’ang’anizi na ndiyo maana tumepiga kombati. Yaani unakataliwa lakini unang’ang’ania.”
Mdee amesema, yeye pamoja na wenzake wanatambua mchango mkubwa wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe “kwangu mimi binafsi, huwezi kumzungumzia Halima bila kumtaja Mbowe na wenzangu kwa nafasi zao. Tunamheshimu sana Mbowe.”
“Mimi na wezangu tumechukuliwa hatua na kamati kuu, niwahakikishe, mimi na wenzangu tutabaki kuwa wana Chadema kindaki ndani. Mimi dhamira ya kuondoka Chadema haipo. Pamoja na changamoto tunayopitia, Halima mnayemfahamu miaka yote, ni yuleyule na nikisema Halima na timu yangu yote,” amesema.
“Kati ya wanawake 19 na 15 waligombea kwenye majimbo na walifanya vizuri sana na kama uchaguzi usingekuwa na sintofahamu nyingi kama kwangu Kawe, wote tungekwenda mjengoni,” amesema
Katika mkutano huo, Mdee amesema “mimi ni mhanga kweli kweli wa siasa za mageuzi, nitakuwa mwendawazimu jana nimesema, uchaguzi ulikuwa hivi, halafu nije nikubaliane na haya. Haya tunayopitia ni changamoto za kisiasa tu.”
“Wanasema Mdee na wenzake, mimi nakubali kupigwa mawe yote, lakini niwahakikishie wana Chadema, kama nimepewa hela na rushwa haina siri na hakuna yoyote na kama kuna mambo yalitokea, yalikuwa na dhamira njema kabisa,” amesema
“Mimi Halima Mdee, sijawahi kununuliwa na sitanunuliwa na sitarajii kununuliwa. Watu wanaofanya kazi na mimi, iwe kwenye chama kwa miaka 16, iwe bungeni kwa miaka 15, wanajua taja watu watatu ambao rushwa kwao ni mwiko, nawezekana nikawa wa kwanza,” amesema
Mdee amesema, yeye pamoja na wenzake, “hatutaondoka Chadema, tutaendelea na taratibu za ndani za kuzimaliza. Tutaendelea kuwa wana Chadema wa hiali na tutaendelea na taratibu za kukata rufaa. Katika mapambano ya siasa, huwezi kuacha kumtaja (Freeeman) Mbowe.”
Mbali na Mdee kufukuzwa, wengi ni wale waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Ester Bulaya na Esther Matiko. Katibu Mkuu wa Bavicha, Nusrat Hanje. Katibu Mkuu Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Grace Tendega.
Makamu Mwenyekiti Bawacha (Bara), Hawa Mwaifunga. Naibu Katibu Mkuu Bawacha, Jesca Kishoa na Katibu Mwenezi Bawacha, Agnesta Lambat.
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa Mtwara, Tunza Malapo, Ceciia Pareso, Asia Mwadin Mohamed, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Siyao.Salome Makamba, Anatropia Theonest na Conchesta Lwamlaza.
from UDAKU SPECIAL BLOG https://ift.tt/3lpyxFQ
via IFTTT
Comments
Post a Comment