Diamond aibuka na sakata mtoto wake kupewa mwanaume mwingine

Dar es Salaam. Wakati sakata la yupi baba mzazi wa msanii wa muziki, Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz likiwa bado vichwani mwa watu, msanii huyo ameibuka na kufunguka kuwa hata yeye ana mtoto ambaye mzazi mwenzie amegoma kumpatia na huenda ameshapewa baba mwingine.


Diamond alisema hayo kupitia mahojiano aliyoyafanya na kipindi cha The Switch cha Wasafi FM, Januari 28 baada ya kuulizwa anadhani ana watoto wangapi.


Akijibu, Diamond alisema anachojua ana watoto sita, tofauti na watu wengi wanavyofahamu kwamba ana watoto wanne ambao ni Tiffah na Nillan aliozaa na Zarina Hassan “Zari”, Dylan aliyezaa na mwanamitindo Hamisa Mobetto na Naseeb Junior aliyezaa na mwimbaji kutoka Kenya, Tanasha Donna.


“Watu wengi wanafahamu mtoto wangu wa kwanza ni Tiffah, lakini ninao wengine wawili ambao walizaliwa kabla yake. Kuna mmoja yuko Mwanza, mama yake amegoma kunipa, pia juzi kati nimeletewa mtoto mwingine wa kike hapa hapa Dar es Salaam, lakini sijawahi kumuona.


“Mama wa huyo mtoto yuko katika mahusiano mengine na mwenye mahusiano naye anajua ni mwanae. Mambo yale...kwa hiyo yule mama anaogopa kuniletea mtoto kwa sababu akikutana na mimi mtoto ataenda kusema kwa baba yake tumeenda kwa Diamond. Kwa hiyo mtoto yupo, inatafutwa timing siku moja kumuona, lakini mama yangu amemuona na akaniambia, mwanangu, yule mtoto ni wako, mmefanana sana,” alisema mkali huyo wa wimbo “Waah”.


Alisema ikiwa watoto hao wawili ni wa kweli, Tiffah atakuwa mtoto wa tatu kwa kuzaliwa.



Sakata la nani baba mzazi wa msanii huyo lilipoanza kuvuma mapema mwezi huu, mama mzazi wa Diamond aliweka bayana baba wa msanii huyo ni mzee anayefahamika kwa jina la Salum Iddi Nyange na sio Abdul Juma kama ilivyokuwa inafahamika awali.


Jambo hilo liliibua mjadala kwa mashabiki na wafuatiliaji wa matukio ya kuvutia ya familia hiyo ikiwemo huenda hakukuwa na uhusiano mzuri kati ya mama Diamond na baba mzazi wa msanii huyo ndiyo maana akamkabidhi mtoto kwa baba mwingine ambaye ndiye huyu mzee Abdul.


Hii inamaanisha matukio yanajirudia ukilinganisha na hiki kinachotokea sasa kwa Diamond kutopewa mtoto wake ambaye anadai yupo Dar es Salaam.


Diamond alifafanua kuwa “Mama akiniambia kitu huwa hadanganyi kwa sababu macho yake ni kama teknolojia inayotumika viwanjani kuhakiki usahihi wa mpira ulipo (VAR), alipomuona aliniambia ni wangu, nasubiri nimuone,” alisema.


Diamond pia alielezea kuhusu sakata la nani baba yake halisi kwa kusema kuwa “Nimefahamu kuwa mzee Abdul siyo baba yangu tangu mwaka 2000, alienieleza ukweli alikuwa mama yangu mkubwa (mama yake Rommy Jones).


“Nilikuwa napenda sana kumtajataja baba yangu, kipindi hicho alikuwa ameshaondoka nyumbani, ametuacha Tandale. Sasa ilikuwa inawaudhi watu akiwemo mama mkubwa kwa sababu alikuwa hatuhudumii wakati alikuwa vizuri kiuchumi. Enzi hizo alikuwa na magari na pesa za kutosha.”


Hilo siku moja lilimkera mama yangu mkubwa na ndipo kwa hasira akamueleza ukweli kuwa baba yake mzazi sio Abdul anayemtajataja kila kukicha, bali ni mtu mwingine anayeitwa Salum Iddi au Salum Bubu kwa jina la utani.


“Ndipo akaniambia kama unakata kuthibitisha nenda pale Tandale sokoni wanapouza mchele wa jumla. Kamuulize mtu anayeitwa Salum Bubu, halafu mwambie mimi mwanao.” alisema.


Diamond alisimulia kwamba alienda huko na kweli akakutana na baba yake.


“Baba akanipa mchele na shilingi mia mbili. Nikapeleka mchele nyumbani mia mbili nikatumia. Na tangu hapo huo ndiyo ukawa mchezo wangu. Nikawa naenda kazini kwa baba mara kwa mara.” Alisema ile kwenda mara kwa mara kwake ikarudisha ukaribu wa mama yake na Salim Nyange na baadaye mzee huyo akampeleka Diamond nyumbani kwake Kariakoo alipokuwa akiishi kwenda kumkutanisha na ndugu zake.


Diamond alifafanua kuwa hata shughuli zake za muziki alianza akiwa Kariakoo alipokuwa akienda na kuishi mara kwa mara kwa baba yake.



from UDAKU SPECIAL BLOG https://ift.tt/2MI66r2
via IFTTT

Comments

Popular posts from this blog

What Happened To Sarafina Skin? From Brown To White Skin – How Did It Happen? Explore The Real Story

MASHAIRI MATAMU YA MAPENZI