Lipumba agusia Katiba Mpya, mikutano ya hadhara siku 100 za Rais Samia
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amemzungumzia siku 100 za utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan akisema kuna baadhi ya maeneo ikiwemo ushirikiano wa kimataifa na haki za binadamu amefanya vizuri.
Amesema maeneo mengine ni sekta za biashara ambapo amekutana na wadau wa sekta hiyo na kujadili masuala mbalimbali, kukiri Tanzania kuna ugonjwa wa corona pamoja na hatua alizozichukua na kuwachukulia hatua watendaji mbalimbali serikalini.
Amesema jambo ambalo hajaridhika nalo ni kauli ya kiongozi mkuu huyo wa nchi kutolitilia mkazo suala la Katiba Mpya na mikutano ya hadhara akisema demokrasia inakwenda sambamba na ujenzi wa uchumi.
Profesa Lipumba ambaye ni mtaalamu wa uchumi, ameeleza hayo leo Jumatano Juni 30, 2021 wakati akizungumza na wanahabari kuhusu siku 100 za Rais Samia pamoja na mipango mikakati ya baadaye ya chama hicho.
"Amekuwa tofauti na mtangulizi wake na kuna mabadiliko ameyafanya ndani siku 100 ikiwemo kumuondoa aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya aliyekuwa akilalamikiwa. Pia amemuondoa aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania ( TPA), Deusdedit Kakoko.”
"Nilikuwa na matumaini makubwa na Rais Samia ndio maana CUF inakwenda kwenye mialiko mbalimbali ya Serikali inayoalikwa kuonyesha tunamuunga mkono. Kilichonisikitisha ndani ya siku 100 ni kigugumizi chake kukutana na vyama vya siasa na suala la Katiba Mpya," amesema Profesa Lipumba.
from Udaku Special https://ift.tt/3hpFlmV
via IFTTT
Comments
Post a Comment