Lyamuremye Jean Claude ahukumiwa miaka 25 jela kwa mauaji ya kimbari Rwanda
Mahakama mjini Nyanza kusini mwa Rwanda imetoa hukumu ya kifungo cha miaka 25 jela dhidi ya Bwana Jean Claude Iyamuremye maarufu Nzinga’ baada ya kumpata na hatia ya mauaji ya kimbari.
Jaji wa mahakama hiyo alisema Lyamuremye alishiriki katika mashambulio yaliyofanywa na makundi ya wanamgambo Interahamwe katika maeneo mbali mbali mjini Kigali ambako maelfu ya watutsi waliuawa.
Lyamuremye mwenye umri wa miaka 46 alisema hangeliweza kushiriki mauaji dhidi ya watutsi ,kabila la mama yake.
Katika kesi ya leo ya kutoa hukumu,mahakama imesema ushahidi ulionesha wazi kuwa wakati wa mauaji ya kimbari alikuwa akitembea na silaha mbali mbali pamoja na wanamgambo Interahamwe kwa lengo la kuwinda na kuwaua watutsi.
Jaji wa mahakama ya mjini Nyanza amesema kwamba Iyamuremye alistahili hukumu ya kifungo cha maisha kama ilivyokuwa imependekezwa na mwendesha mashtaka lakini kwamba hukumu hiyo ilipunguzwa hadi kifungo cha miaka 25 jela kutokana na kwamba makosa aliyofanya akiwa na umri wa miaka 19 ambao ni umri wa ‘kushawishika’.
Kadhalika Jaji amesema ‘’pamoja na kuwa alishiriki mashambulio dhidi ya watutsi kuna watutsi wengine aliowasaidia kuokoa maisha yao’’.
Lyamuremye Jean Claude alirudishwa Rwanda na nchi ya Uholanzi mwaka wa 2016 ili kukabiliana na mashtaka ya mauaji ya kimbari .
Alikamatwa na kuzuiliwa Uholanzi mwaka 2013 alipokuwa dereva wa watumishi wa balozi za Israel na Finland .
from Udaku Special https://ift.tt/3hjV8Uf
via IFTTT
Comments
Post a Comment