JICHO LA MWEWE: Haji Manara ni ‘Malaika au Shetani’?



HAJI Manara anaingia katika rekodi ya aina yake nchini. Rekodi ambayo unaweza kuiweka katika kitabu cha rekodi ya maajabu ya dunia cha Guiness. Anakuwa kiongozi wa kwanza kukatisha boda baina ya klabu mbili kubwa nchini, Simba na Yanga.

Mastaa wengi waliocheza soka zamani waliwahi kukatisha boda katika klabu hizi. Kina Omary Hussein ‘Keegan’, Mohammed Hussein, Juma Kaseja, Hamis Gaga, Zamoyoni Mogella, Athuman Idd ‘Chuji’, Said Mwamba ‘Kizota’, Edibily Lunyamila, Athuman China, Godwin Aswile, Willy Martin, Nico Bambaga, Seleman Mathew, Ally Yusuf ‘Tigana’ na wengineo.

Haijawahi kutokea kiongozi akakatisha boda. Haijawahi kutokea kiongozi akavuka mpaka huu wa kutoka Simba kwenda Yanga au kutoka Yanga kwenda Simba. Awe kiongozi wa kuchaguliwa au kiongozi wa kuajiriwa. Hapa nazungumzia wazawa. Haji anakuwa wa kwanza. Kwa wageni, Senzo Masingiza alishtua mwaka jana.

Kwanza kabisa hizi klabu zina tamaduni zake. Hata ukiwa dereva wa basi wa Yanga unapaswa kuwa shabiki wa Yanga. Ukiwa mfagiaji wa ofisi za Simba unapaswa kuwa Simba. Na sasa imekwenda hadi katika mauzo ya hisa. Ukitaka kununua hisa za Simba lazima uwe Simba. Na Yanga itakuwa hivyohivyo.


 
Usimba na Uyanga unakaa katika damu. Ni kigezo cha kwanza pia. Hauaminiki mpaka uwe Yanga au Simba. Baada ya hapo mengine huwa yanafuata. Haji ametuweka kwenye mtego wa maamuzi kuhusu namna ya kumhukumu.

Unaweza kutazama suala la Haji katika sura tatu. Sura ya kwanza ni kwamba Haji ni raia mwenye hasira kwa sasa dhidi ya waajiri wake wa zamani. Hakuondoka Simba kwa amani. Ameondolewa na hasira zimemjaa kupitiliza.

Inawezekana amefanya alichofanya kwa ajili ya kulipiza kisasi. Kwa sasa anatamba mitandaoni akiwa na jezi za njano na kijani. Maudhi yake ni yaleyale ambayo zamani watu wa Yanga walikuwa wanayakabili akiwa na Simba. Sasa ni zamu ya watu wa Simba.


Kwa sasa anaweza kufanya mara mbili zaidi kwa sababu ya kuwaonyesha waajiri wake wapya kwamba yeye ni mwenzao na kule ameondoka na hana mpango wa kugeuka nyuma au kuwauza. Nadhani kwa sasa atakuwa ‘Yanga’ kuliko ‘Yanga wenyewe’.

Tukiachana na hilo, inawezekana pia Yanga wakanufaika na Haji kwa ajili ya kuwaongezea utamu wa klabu yao. Ataipamba Yanga kupitiliza kama alivyokuwa anaipamba Simba na timu itatengneeza mvuto hata kwa vijana wadogo. Lakini hili zaidi litachangiwa na ubora wa timu yenyewe.

Simba na Haji vyote vilibebana. Mastaa wa Simba walimbeba Haji kwa sababu mdomo wake ulikuwa unapewa sapoti na uwezo mkubwa wa kitimu wa Simba na mastaa wake. Haji asingeweza kutamba sana na Simba kama washambuliaji wake wangekuwa kina Michael Sarpong.

Jambo la tatu ambalo ni muhimu kulichunguza na kujua ni kwamba huenda pia hatua ya Yanga kumchukua Haji ikawasaidia watu wengine ambao watavuka boda siku zijazo kwa sababu za kiajira zaidi na weledi wao (professional) bila ya kujali mapenzi yao yako wapi.


 
Kwa mfano, vipi baada ya kila kitu kilichotokea bado Haji akafanya kazi safi akiwa na Yanga kiasi kwa-mba timu ika-endelea kung’ara bila ya matatizo yoyote. Hivi ni kweli kwamba hata daktari wa timu ya Yanga anapaswa kuwa shabiki wa Yanga?

Vipi kama itatokea kuna daktari mzuri mtaalamu ambaye wanaweza kuwa naye, lakini ni shabiki wa Simba? Haitawezekana kumchukua? Nadhani hofu kubwa zaidi ni hujuma dhidi yao. Hofu hii imemeza ukweli kwamba kuna vitu inabidi vifanyike kiweledi bila ya kujali mapenzi.

Baada ya miaka kadhaa huenda Haji akawa amefungua milango ya ufanyaji kazi kiweledi zaidi bila ya kujali mapenzi. Yanga wamechukua ‘risk’ hii, lakini Haji mwenyewe amechukua ‘risk’ hii kwa sababu akifanya vyema katika klabu ya Yanga huenda akawa ameng’oa mzizi wa fitina.

Wachezaji waliowahi kuhama Simba kwenda Yanga au kuhama Yanga kwenda Simba wengi wao walifanya kazi nzuri. Said Mwamba alikuwa Yanga hasa na alilelewa na Yanga tangu alipotoka kwao Kigoma, lakini lilipofika suala la kazi yake aliifanya vyema wakati alipohamia Simba. Aliwahi kuwafunga bao pia.


Kina Mogella na Gaga walifanya kazi nzuri walipokwenda Yanga ingawa walikuwa Simba. Mogella alichukua ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati pale Uganda akiwa na Yanga huku uwanjani akifanya majukumu yake kiufasaha kiasi cha kuitwa jina la DHL.

Hiki ndicho kinachomkabili Haji kwa sasa. Kama akifanya kazi yake kwa ufasaha basi huenda akawafungulia milango watu wengine wakafanya kazi zaidi katika klabu hizi bila ya kujali mapenzi. Awali ilionekana kitu kisichowezekana kiasi kwamba taaluma nyingine muhimu kama ukocha pia imekosa watu wa aina hii.

Ni hayati Joel Bendera na Syllersaid Mziray tu ndio wanaobaki kuwa makocha pekee wa wazawa kuwahi kufundisha Simba na Yanga kwa vipindi tofauti. Baada ya hapo na hadi sasa hakuna kocha wa mzawa aliyewahi kuweka rekodi hiyo ingawa tunafahamu kwamba taaluma hiyo huwa inabeba watu wenye weledi na ambao hawapendi kusaliti timu zao.

Wachezaji wanaweza kusaliti timu lakini ni nadra kwa makocha kufanya hivyo, lakini bado mpaka sasa makocha hawaaminiki.

Uzuri wa Haji ni kwamba wakati mwingine hatapata wakati mgumu sana kufanya kazi na watu wa Yanga kwa sababu alilelewa na Yanga. Baba yake Mzee Sunday Manara alikuwa staa wa Yanga. Haji alikuwa anacheza na watoto wenzake wa Yanga kando ya Uwanja wa Kaunda kabla ya baba yake hajaanza mazoezi.


 
Haji atakuwa ‘malaika’ au ‘shetani’? Huku Simba alionekana kama malaika lakini sasa hivi ataonekana kama shetani. Kule Yanga pia alionekana kama shetani lakini sasa anaonekana kama malaika. Nilichopenda ni namna ambavyo amefanikiwa kuviyumbisha vichwa vya mashabiki wa soka nchini.


from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/3Dnd3U2
via IFTTT

Comments

Popular posts from this blog

MASHAIRI MATAMU YA MAPENZI

What Happened To Sarafina Skin? From Brown To White Skin – How Did It Happen? Explore The Real Story