Mama, Dada wa Hamza waachiwa, watano bado, Mwili wa Hamza Ulitolewa Risasi Kabla ya Kuzikwa
Dar es Salaam. Wakati mama na dada wa marehemu Hamza Mohammed wakiachiliwa baada ya mahojiano, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema bado wanaendelea na upelelezi wa tukio hilo.
Hamza aliuawa na polisi Agosti 25, mwaka huu baada ya kuwaua kwa risasi askari wanne, watatu kati yao wa polisi na mmoja wa kampuni binafsi ya ulinzi, jirani na ulipo Ubalozi wa Ufaransa jijini Dar es Salaam.
Kufuatia tukio hilo Jeshi la Polisi liliwakamata ndugu kadhaa wa Hamza waliokuwa jijini na Dar es Salaam na wengine Chunya mkoani Mbeya.
Hata hivyo, alipoulizwa na Mwananchi kuhusu watu waliokamatwa kutokana na tukio hilo jana, Kamanda Muliro alisema; “Jamani nyie hamtaki tupeleleze? Ni sahihi tuseme hadi wapo mahabusu namba ngapi? Ametoka au hajatoka? Ndugu yangu Mwananchi!”
Wakati Muliro akisema hayo, Msemaji wa familia ya Hamza, Abdul-rahman Hassan aliliambia Mwananchi kuwa watu takribani saba wakiwamo mama na dada wa Hamza wameachiwa na wengine watano wanaendelea kushikiliwa na polisi.
Hayo yamebainika ikiwa ni siku moja, baada ya mwili wa Hamza kuzikwa juzi usiku katika makaburi ya Kisutu Jijini Dar es Salaam.
“Kati ya waliokuwa wamekamatwa ndugu walikuwa mama na dada yake tu, wengine ni marafiki na jamaa. Walioachiwa ni kama saba na wengine watano bado wanaendelea na mahojiano na polisi...,” alisema Hassan.
Gazeti hili jana lilimnukuu Hassan, nduguye Hamza, akidai walichelewa juzi kuzika hadi usiku kwa sababu mwili huo ulikuwa unatolewa risasi.
Alipoulizwa kuhusu idadi ya risasi zilizotolewa kwenye mwili huo jana, Kamanda Muliro alisema hawezi kujibu swali hilo, bali anachofahamu ni kuwa juzi polisi walikabidhi mwili huo kwa ndugu zake kwa ajili ya maziko.
“Itoshe kujua mwili wao tuliwakabidhi, sasa kama wamezika au hawakuzika, kuna maswali ni yangu, mengine sio ya kwangu. Sawasawa uniulize wamezika au hawakuzika, sasa nitakujibu nini hapa,” alisema Muliro.
Hata msemaji wa familia hiyo alisema hawezi kujua mwili wa Hamza ulikutwa na risasi ngapi ingawa alisema walichelewa kuuzika kwa sababu ulikuwa ukitolewa risasi.
Mwili huo ulitakiwa kuzikwa saa 7 mchana, lakini ukazikwa saa mbili usiku.
Hatua ya mwili huo kuzikwa usiku inaelezwa na Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka kuwa ni ya kawaida, kwa kuwa utaratibu wa kuzika unafanyika wakati wowote ilimradi makaburi husika yawe na taa, akisema hilo ndiyo jambo muhimu katika maziko.
Sheikh huyo anafafanua kuwa ikiwa mwili wa marehemu una kitu kinachowezekana kutolewa kinatakiwa kutolewa kabla ya kuzikwa.
“Lakini kama hakiwezekani kinaachwa. Mfano maiti ya ajali yenye vyuma vimemuingia, watafanya kila liwezekanalo kuondolewa, hawezi kuzikwa navyo na ndivyo walipoona kuna risasi imemuingia waliitoa,” alisema Sheikh Mataka aliyeongoza mazishi ya Hamza.
Hakuacha mke, mtoto
Katika hatua nyingine, Msemaji huyo wa familia alisema Hamza hakuacha mke wala mtoto na wakati wote alikuwa akiishi na mama yake eneo la Upanga na kila aliporudi kutoka Mbeya alifikia pale.
“Hana mke wala mtoto, alikuwa akija anafikia kwa mama yake, anakaa wiki mbili, tatu au moja anaondoka kwenda Mbeya kwenye shughuli zake.
Kuhusu vitu vilivyobebwa na jeshi la polisi siku walipofanya ukaguzi alisema hana uhakika ni vitu gani huku akibainisha kuwa ni vile vilikuwa vinahusiana na Hamza.
Uchunguzi wa kina
Agosti 27, 2021 katika ibada ya kuaga askari waliopoteza maisha katika tukio hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani George Simbachawene alisema uchunguzi wa kina utafanyika ili kubaini sababu za Hamza kufanya mauaji hayo na taarifa rasmi itatolewa ikiwa na mapendekezo ya nini kifanyike kwa siku za usoni yanapotokea matukio yanayofanana na hilo.
Siku moja baadaye Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Simon Sirro alisema mwili wa Hamza watawakabidhi ndugu zake baada ya polisi kumaliza kazi yao wameshaufanyia kazi.
from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/3jr4u2G
via IFTTT
Comments
Post a Comment