Prof. Ndalichako aonya urasimu wakati wa kusajili bunifu za Teknolojia zinazoibuliwa hapa nchini






Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma.
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amezitaka taasisi zinazohusika na utambuzi na kusajili wabunifu wa teknolojia hapa nchini kuondoa urasimu katika zoezi la kusajili wabunifu na bunifu zao ili kuongeza hamasa kwa wabunifu wengi kujitokeza.

Pia amebainisha kuwa serikali imetenga bilioni 43 ili kulea wabunifu mbalimbali katika vituo atamizi vilivyopo katika vyuo vya elimu ya juu vinavyotumika kulea wabunifu wanaoendelea kuibuliwa hapa chini.

Waziri Prof. Ndalichako ameyabainisha hayo leo Augost 30, 2021 Jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri zote hapa nchini kikao chenye lengo la kuwajengea uwezo wa kuibua na kuzitambua bunifu za teknolojia katika maeneo yao ya kazi.

Ambapo amesema vitendo vya urasimu katika zoezi hilo vinafifisha na kukatisha tamaa wabunifu wengi wa teknolojia kujitokeza kujisajili na ili bunifu zao ziweze kujulikana na wao kunufaika na bunifu zao katika kurahisisha kazi mbalimbali kupitia bunifu hizo.

“Sisi kama serikali tuna tambua mchango mkubwa wa bunifu za teknolojia kwa mwaka huu wa fedha sisi tumetenga bilioni 43 hizi zitakwenda kuboresha mazingira na kutumika kuwaendeleza wabunifu katika vituo atamizi vilivyopo katika vyuo vikuu mbalimbali,

Tuna vyuo kama Chuo Kikuu cha Dar es saalam UDSM, Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine, Mandela, Mzumbe, na Chuo cha Sayansi na Teknolojia Mbeya MUST ni miongoni vya vyuo ambavyo vinatumika kulea wabunifu tunaowaibua katika mashindano ya MAKISATU” amesema Prof. Ndalichako.

Ameongeza kuwa “ Ndio maana tumewaita hapa ninyi ndio mnakuwa na watu tangu ngazi za chini tunaamini kupitia kwenu tunaweza kupata wabunifu wengi sana hasa wabunifu ambao wapo nje ya mfumo rasmi ninyi mnaweza kuwapata kiurahisi” amesema.

Prof. Ndalichako amesema hatamani kuona wabunifu wanaibuka katika ziara ya viongozi wa ngazi za juu na kuonyesha bunifu zao na kuomba msaada wakati Wizara hiyo imeendaa utaratibu mzuri wa kuwatambua wabunifu katika ngazi zote na hatimaye kuweza kunufaika na bunifu zao.

Amewataka Maafisa maendeleo ya jamii hao kwenda kuwa chachu katika kuwaibua wabunifu wa Teknolojia katika maeneo yao na kuwaeleza umuhimu wa bunifu zao kwa maendeleo ya taifa na uchumi wa mtu mmoja mmoja.

Amesema Wizara iliona kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na teknolojia na ikaanzisha mashindano ya kutafuta wabunifu wa teknolojia mashindano yaliyofahamika kama MAKISATU ambayo yanatumika kuibua na kuendeleza bunifu mbalimbali hapa nchini.

Amesema tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo mwaka 2019 tayari wameibua wabunifu 1785 na kati ya wabunifu hao bunifu 130 zinaendelezwa kupitia tume ya taifa ya sayansi na teknolojia COSTECH na teknolojia 389 zilitambuliwa na kuhakikiwa taarifa zake.

Awali Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe amesema anaamini kwa msaada wa maafisa maendeleo ya jamii kupitia mafunzo hayo wataweza kuwa na wigo mpana zaidi wa kuibua teknolojia mbalimbali hapa nchini.

Pia amebainisha kuwa wataendelea kutoa mafunzo kama hayo hadi kwa maafisa maendeleo ya jamii ngazi ya kata, na walianza na maafisa maendeleo ngazi za Mikoa na sasa halmashauri wanaamini watafika hadi ngazi za kata.

Kwa upande wake Kaimu rais wa chama cha maafisa maendeleo ya jamii hapa nchini bwana Wanchoke Chinchibera amesema baada ya kupata mafunzo hayo watakwenda kulifanya jukumu hilo kwa ufasaha mkubwa kuhakikisha wanawaibua wabunifu wengi wa teknolojia kwa maendeleo ya taifa.

“Tuwahakikishie kuwa tutakwenda kuifanya kazi hii kiufasaha na tutakwenda kuhamasishana kupitia chama chetu kuhakikisha tunaibua bunifu nyingi katika maeneo yetu ya kazi” amesema Wanchoke.

 


from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/3DvxaiP
via IFTTT

Comments

Popular posts from this blog

What Happened To Sarafina Skin? From Brown To White Skin – How Did It Happen? Explore The Real Story

MASHAIRI MATAMU YA MAPENZI