Samia "Tutaliangalia Hili la Matokeo Masomo ya Dini na Kutotambulika Kwa Vyuo Vinavyofundisha Masomo ya Biblia na Theolojia"

 


Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inakwenda kuliangalia suala la kutotambuliwa kwa vyuo vinavyofundisha masomo ya Biblia na theolojia katika mabadiliko ya sera ya elimu yanayofanyika sasa.

Ametoa kauli hiyo jijini Dodoma, wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya kuanzishwa kwa Kanisa la Anglikana Tanzania yaliyokwenda sambamba na kongamano la maaskofu na wachungaji wa kanisa hilo.

Kauli hiyo ilitokana na ombi la Askofu Mkuu wa Anglikana Tanzania, Dk Maimbo Mndolwa la kutaka Serikali kutambua elimu ya dini inayotolewa katika vyuo vinavyomilikiwa na kanisa hilo nchini.

Dk Mndolwa alibainisha mambo mbalimbali ambayo kanisa lake linafanya katika sekta za afya, elimu na ulinzi, huku akiiomba Serikali pia iangalie suala la kodi katika huduma zinazotolewa na taasisi za dini.

Rais Samia alisema Serikali imelichukua suala la kutotambuliwa kwa vyuo vya kufundishia Biblia na Theolojia na baadaye watatoa mrejesho wa suala hilo.

“Niseme tunayachukua, tutayaangalia na tutaleta mrejesho. Hii siyo kwa Anglikana pekee, ni kwa taasisi za dini zinazofundisha dini zote, bado hatujaziweka kuzitambua kwenye mitaala yetu au tunapofanya tathmini ya kuhitimu watoto wetu wa Kitanzania.

“Kwa hiyo tunapokwenda kuiangalia sera ya elimu ambayo tunaiangalia sasa, tutakwenda kuliangalia tuone uzito wake halafu tutaleta mrejesho kwa dini zote na madhehebu yote,” alisema kiongozi huyo.

Wakati huohuo, Rais Samia aliwataka viongozi wa dini kuwahimiza wananchi kwenda kupata chanjo ya Uviko-19 sambamba na kushiriki sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwakani.

Alisema imezoeleka Serikali ikitoa matamko ya shughuli kama hizo, anatokea kiongozi wa dini anaanza kupinga wakati mafundisho ya kwenye kitabu chake hayamtumi kufanya hivyo.

“Naomba sana, nendeni mkatuhimizie zoezi la sensa, lakini pia mpige kampeni ya kutosha kwenye suala la Uviko-19. Ukweli ni kwamba chanjo zinapunguza vifo, lakini pia inapunguza makali ya lile gonjwa,” alisema Rais Samia.

Alisisitiza kwamba viongozi wa dini wawaelimishe waumini wao ili wakubali kuchanja kwa hiari yao baada ya kuelimishwa na kuelewa kwamba wakichanja watapata nini na asipochanja anakosa nini.

Hata hivyo, kauli hii ya Rais inakuja ikiwa ni siku mbili tu kupita, alipotoa maelekezo ya kuanza kufanyika kampeni ya kitaifa ya kuelimisha jamii kuhusu chanjo ya Uviko-19 alipokuwa akizindua mkutano mkuu maalumu wa ALAT jijini Dodoma.

Rais alisema kwa kufanya hivyo, kutasaidia wananchi wahamasike kuchanja.

Alitaka ushirikishwaji wa makundi mbalimbali upewa kipaumbele kwenye kampeni hiyo.

Lakini pia jana watumiaji mbalimbali wa simu za mkononi walianza kupokea ujumbe mfupi unaohamasisha watu kuchanja.

Ujumbe huo unasomeka, “Chanjo ya Uviko-19 itakukinga na ugonjwa, kulazwa na hatari ya kifo. Fanya uamuzi wa kupata chanjo. Wahi sasa okoa maisha”

Usawa wa kijinsia

Kuhusu usawa wa kijinsia, Rais Samia alilitaka Kanisa la Anglikana kuwekeza nguvu katika kujenga heshima ya mwanamke wa Kitanzania.

Alisema Serikali imedhamiria kwa dhati kuwainua wanawake kijamii, kiuchumi na kisiasa na pia kupambana na ukatili, kejeli na manyanyaso dhidi ya wanawake na watoto.

“Tunafanya hivyo siyo kwa ajili mimi ni Rais mwanamke, la hasha. Tunafanya hivyo kwa sababu mwanamke ni kiumbe mwenye haki sawa na kiumbe mwingine anayezaliwa na mwanadamu.

“Wote tunazaliwa sawa, kinachotutofautisha ni makuzi na imani katika makabila yetu na imani mbalimbali. Kwa hiyo mwanamke ana haki sawa na mwanamume katika jamii,” amesema Rais Samia.

Awali akizungumza kwenye maadhimisho hayo, Dk Mndolwa aliitaka serikali kwenda kuangalia suala la kodi kwa taasisi za dini kwa jicho la huruma kwa sababu inatishia baadhi yao kutaka kufunga huduma.

Pia, aliitaka serikali iboreshe mifumo ya utoaji vibali vya huduma mbalimbali, mathalani vibali vya kuanzishwa kwa dayosisi na vibali vya kuanzisha vituo ili viendelee kufanya kazi kwa manufaa ya wananchi.

“Kuna changamoto ya kanisa kutakiwa kulipa kodi kiasi zinazotishia kufunga baadhi ya huduma zetu. Sisi tunafanya ni ibada, mfano hospitali na shule za jamii, pamoja na kwamba zinatoa huduma, lakini zinatakiwa kulipa kodi kwa serikali na kodi nyingine ambazo haziendani kabisa na mapato ya hospitali.

“Tunafurahi kwamba Serikali yako inayaangalia masuala haya, lakini tukuombe utuangalie kwa jicho la huruma kwa sababu inapelekea baadhi ya taasisi hizi kustruggle sana katika kujiendesha,” alisema Askofu Mndolwa.

Akijibu hoja hiyo, Rais Samia alisema ameagiza watu wake kufanya tathmini upya ili kubaini taasisi za dini zinazotoa huduma na zile zinazofanya biashara.

Alisema taasisi zinazofanya biashara lazima zilipe kodi katika sehemu ya faida wanayoipata.



from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/3kVXHPf
via IFTTT

Comments

Popular posts from this blog

What Happened To Sarafina Skin? From Brown To White Skin – How Did It Happen? Explore The Real Story

MASHAIRI MATAMU YA MAPENZI