Harmonize Amfanyia Ukorofi Kiba
HUU ni ukorofi kama ule wa Mama Tariki! Hivyo ndivyo wasemavyo baadhi ya mashabiki kufuatia kitendo cha msanii mwingine wa kimataifa wa Bongo Fleva, Rajab Abdul au Harmonize kutanganza ujio wa albam yake aliyoipa jina la High School atakayoiachia Novemba 5, mwaka huu.
Harmonize au Harmo alitoa tangazo hilo juzi, Jumatano, Oktoba 27, mwaka huu; siku chache baada ya msanii mwenzake, Ali Saleh Kiba au King Kiba kuachia albam yake ya Only One King.
Albam ya Hamonize au Konde Boy Mjeshi ina nyimbo kali zipatazo 20 ambapo tatu kati ya hizo amewashirikisha wakali kutoka nje ya Bongo; Why aliyomshirikisha Sarkodie, Mood aliyomshirikisha Naira Marley na Sandakalawe aliyomshirikisha Busiswa.
Nyimbo nyingine tatu amewashirikisha mastaa kutoka Bongo, Mdomo aliomshirikisha Ibraah, What Do You Miss aliomshirikisha Anjella na Kamaliza aliomshirikisha mkali wa muziki wa Singeli, Sholo Mwamba.
Katika albam hiyo ya High School, nyimbo 14 ameimba peke yake na sita amewashirkisha wasanii wengine akitaka kuthibitisha jina lake jipya la Teacher na anataka wanafunzi wajifunze kutoka kwake.
ALBAM YA HARMONIZE
Konde Boy kutoka Mtwara ambaye amesugua mno hadi kutoboa tundu kwenye muziki, kwa mara ya kwanza baada ya kutoka kwenye lebo iliyomkuza inayomilikiwa na bosi wake wa zamani, Chibu Dangote au Diamond Platnumz, Machi 14, 2020 aliachia albam iliyokwenda kwa jina la Afro East ambayo ilitikisa na bado inatisha.
Katika Albam ya Afro East aliwashirikisha wasanii kibao kutoka nje na ndani ya Bongo kama Yemi Alade, Burna Boy, Phyno, Lady Jaydee na wakali wengine.
Albam ya Afro East hadi sasa bado inafanya vyema katika ‘platifom’ za kusikiliza na kununua muziki kama Audio Mack ambapo imesikilizwa mara zaidi ya milioni 13.7.
ALBAMU YA KING KIBA
Mfalme wa Bongo Fleva kama yeye anavyojiita au King Kiba, Oktoba 4, 2021 aliachia albam yake ya Only One King ambayo ndani yake amefanya kolabo kibao na wasanii kutoka nje ya Bongo kama Sauti Sol, Blaq Diamond, Khaligraph Jones na wengine kibao.
Katika albam hiyo ya Kiba kuna nyimbo 16 ambazo zimekwenda shule huku mapokezi yake yakiwa ni makubwa mtaani na kwenye platifom za kusikiliza na kununua muziki kama Audio Mack ambako huko Only One King hadi sasa ina wasikilizaji zaidi ya milioni 8.89 ndani ya muda mfupi.
UKOROFI WA HARMONIZE KWA KIBA
Kitendo cha Harmonize kutangaza ujio wa albam yake ya High School kinatajwa kuwa ni ukorofi kwani hajampa nafasi King Kiba kutawala soko akiwa na albam yake ya Only One King.
Hata mwezi mmoja bado haujatimia tangu King Kiba aachie albam yake hiyo inayofanya vizuri, Harmonize amekuja na albam yake atakayoiachia Novemba 5, 2021.
UKOROFI WA DIAMOND
Wapo baadhi ya mashabiki ambao wanadokeza juu ya uwezekano wa Dianmond Platnumz naye kuingilia ukorofi huo, naye akamfanyia ukorofi Harmonize.
Vyanzo vya ndani vinadokeza kuwa, Mondi ataachia albam yake kabla ya mwaka huu kuisha ili aoneshe ukubwa wake kwenye muziki hivyo huwenda naye akamfanyia ukorofi Harmonize.
SIYO JAMBO GENI
Watu wanaoufuatilia vizuri muziki wa Bongo Fleva wanasema siyo jambo geni, kwani Mondi na wanamuziki wake wa WCB wamekuwa wakiachia ngoma muda mfupi baada ya wasanii wengine wakubwa kuachia ngoma, kama Kiba na Harmonize ili kuwapunguzia spidi.
“Sijui mbinu hii ya kibiashara inaitwaje, lakini hapa tutaiita ukorofi, ndiyo ni ukorofi kwani kuna nafasi ya kuachia ngoma baada ya muda ambao msanii mwingine ameachia.
“Lazima tukubali kuwa muziki wa Bongo Fleva umefika mbali mno, wasanii wetu kuitwa kwenye shoo za nje siyo jambo la kushangaza kwa sasa. Kwani wanakiwasha vya kutosha tu.
“Pia lazima tuukubali ukweli wa kwamba, Kiba, Diamond na Harmonize ndiyo wasanii wakubwa waliobeba wasanii wengi kwenye soko la muziki Bongo kwa sasa, hili halipingiki. Vijana wanafanya vyema mno, vijana wanapamba hasa, hawana sababu ya kufanyiana ukorofi, bali wanachopaswa kufanya kusapotiana,” anasema Sibongile_1 aliyejitambulisha kama shabiki mkubwa wa muziki wa Bongo Fleva.
TAMBO ZA HARMONIZE
Katika tambo zake baada ya tangazo la albam yake hiyo, Harmonize ametamba kwamba, albam hiyo ilikuwa itoke mwezi Juni, mwaka huu, lakini kuna vitu viliingilia kati na mipango haikwenda kama alivyopanga.
Mbwembwe na mikwara ni vitu ambavyo amekuwa akivifanya Harmonize ili kuwaandaa mashabiki wake kufuatilia muziki wake ambapo amewakaribisha wasanii wenzake darasani kwake ili kuwafundisha muziki.
Mbali na hilo ametamba kwamba ni albam ambayo itatikisa duniani kutokana na ubora wake na kwamba anakwenda kuwanyamazisha wasanii kabisa wenzake.
STORI; BAKARI MAHUNDU, DAR
from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/3CxqIXW
via IFTTT
Comments
Post a Comment