Askofu Shoo ataka haki vyombo vya dola


 

Moshi. Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo, amevitaka vyombo vya dola wakiwamo mahakimu na majaji kutenda haki na kuepuka kuwaonea na kuwatesa wengine kwa kufikiri Mungu haoni.


Askofu Shoo aliyasema hayo  wakati akitoa ujumbe wa Krismasi kwenye ibada iliyofanyika katika Usharika wa Moshi mjini akivitaka vyombo na dola kuacha vitendo vyote vya hila vinavyosababisha maumivu kwa wengine.


Katika ujumbe wake huo, Askofu Shoo alivitaka vyombo hvyo kuwatendea haki wananchi.


“Ni wito wangu kwa wazazi, walezi, vyombo vya dola, mahakimu na majaji niwaombe tendeni haki acheni kuwaonea watu, acheni kuwatesa wengine kwa hila mkifikiri Mungu haoni,”alisema Askofu Shoo ambaye pia ni mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini.


Kwa mujibu wa Askofu Shoo, Mungu anaona kilio na huzuni kutoka kwa wale wote wanaoonewa na kwamba anao uwezo na nguvu za kubadilisha machungu na huzuni zao kuwa furaha na furaha za wale wanaowatesa na kuwaonea kuwa huzuni.


“Tuache na kukataa vitendo vyote vya hila vinavyosababisha maumivu kwa wenzetu, tuache kusababisha huzuni kwa wenzetu, Mungu hapendezwi na hali hiyo,”alisema na kusisitiza vyombo vya dola wakiwamo mahakimu na majaji kutenda haki.


“Mungu anawaona tena anakisikia kilio na anaona machozi na huzuni za wale wote wanaoonewa, kama alivyobadilisha huzuni na hofu kwa wale wachungaji, kwa Mungu hili si jambo ngumu, kubadilisha huzuni za wale wanaolia sasa kuwa furaha,”alisema.


Aliongeza: “Vivyo hivyo si jambo gumu kwa Mungu kubadilisha furaha na kicheko cha wale wanaofurahi na kushangilia sasa kuwa kilio na huzuni, tutambue yupo Mungu anayeweza, tujiepushe na hayo ili nchi yetu ibarikiwe.’’


Askofu Shoo alisema kwa kufanya hivyo si kwamba nchi ya Tanzania itabariwa bali hata, familia za Watanzania na kwamba zitaishi kwa amani na furaha na watu wote watafanikiwa katika maisha ya upendo.


Awaasa wenye mamlaka


Alisema wapo watu wanaosababisha huzuni na machungu kwa wengine kwa sababu tu wanayo nafasi, nguvu na mamlaka na kuwataka kuepuka hali hiyo na kuhakikisha wanakuwa sehemu ya furaha na amani kwa wengine.


“Kwa neema ya Mungu tumejaliwa kuiona Krismasi nyingine ya mwaka huu, tuache kusababishiana machungu na maumivu kwa wengine, ukweli ni kwamba wapo watu wanaosababisha wenzao wakose amani,”alisisitiza.


Askofu Shoo alitumia pia nafasi hiyo kukemea vitendo vyote vya kikatili vinavyotokea nchini katika ngazi ya familia na maeneo mengine.


“Tumeona na kushuhudia ukatili wa wazi katika familia, ukatili kwa watoto nyumbani na maeneo mengine, tukemee kwa nguvu zote ukatili wa aina yoyote ile,”alisema Askofu Shoo, kauli ambayo imekuja wakati mkoa ukitikiswa kwa mauaji.


Akihubiri kanisani hapo, Askofu Shoo alisema katika kukumbuka kuzaliwa kwa Yesu Kristo, kila mmoja asukumwe kutenda haki na kusaidia wale wanaoonewa na kwamba kuzaliwa kwa Yesu Kristo kukarejeshe matumaini kwa walioyapoteza.


Alisema kila Mtanzania anapaswa kukataa maovu, vitendo vyote vya chuki, kufanyiana hila, kutendeana mabaya na kila mmoja asafishe moyo wake na mwenendo wake.


Katika siku za karibuni, baadhi ya vyombo vya dola vimekuwa vikinyooshewa kidole kwa uvunjifu wa haki, ikiwamo kubambikia wananchi kesi.


Suala limemgusa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye alishatoa maagizo kwa vyombo hivyo kuacha tabia ya kubambikizia watu kesi.



from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/3mANicb
via IFTTT

Comments

Popular posts from this blog

What Happened To Sarafina Skin? From Brown To White Skin – How Did It Happen? Explore The Real Story

MASHAIRI MATAMU YA MAPENZI