Ripoti Maalum: Bei ya gesi Haikamatiki



"NIMEONA nitumie mkaa kwa sasa mpaka bei ya gesi itakaposhuka, maisha ni magumu. Gesi ya kilo 15 ninayoinunua kwa Sh. 25,000, ninatumia kwa mwezi na wiki moja wakati gunia la mkaa la 27,000 ninalitumia kwa miezi miwili," Tina Shemweta, mkazi wa Ubungo mkoani Dar es Salaam anawasilisha kilio chake.

WAZIRI WA NISHATI, JANUARY MAKAMBA: PICHA MTANDAO
Tina (32), mama wa mtoto mmoja, analalamika kuwa kwa sasa amelazimika kuachana na matumizi ya gesi ya kupikia (LPG) kutokana na kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo kutoka Sh. 20,000 miezi minne iliyopita hadi Sh. 25,000 kwa mtungi mdogo wa ORYX.

Anasema amelazimika kurejea kwenye matumizi ya mkaa kwa kuwa familia yake haiwezi kumudu bei mpya za gesi.

Jamila Mwinchea, mkazi wa Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam, ana kilio kama cha mtangulizi wake Tina, akilalamika kuwa sasa ananunua gesi ya kupikia kwa Sh. 58,000 kutoka Sh. 45,000 miezi minne iliyopita kwa mtungi wa Kg 30 wa kampuni ya ORYX.

"Gesi imepanda sana dada yangu (mwandishi), si mchezo. Kuna ongezeko la Sh. 13,000 kwa kipindi cha miezi minne tu, na inavyoonekana serikali isipoingilia kati itazidi kupaa," anatahadharisha.


Alphonce George, mkazi wa Kimara Baruti wilayani Ubungo, anasema bei ya mtungi wa Kg 30 wa kampuni ya gesi ya Taifa kwa sasa kwenye maeneo yao imefikia Sh. 53,000 kutoka Sh. 45,000 ilivyouzwa awali.

"Yaani wanapandisha halafu wanasikilizia, watu wanalalamika wakiona wameacha wanapandisha tena. Yaani tumetoka kununua kwa Sh. 45,000 mpaka Sh. 53,000 sasa. Tunaiomba serikali iingilie kati kutunusuru, hali ya maisha ni ngumu," analalama.

Jana mchana, Nipashe ilipita kwenye maduka yanayouza nishati hiyo maeneo ya Mwenge wilayani Kinondoni na kukuta mtungi wa Kg 15 wa gesi ya ORYX unabadilishwa kwa Sh. 24,000 na Kg 30 Sh. 58,000 wakati gesi ya Taifa Kg 15 unabadilishwa kwa Sh. 22,000 na Kg 30 Sh. 54,000.


Rose James ni muuzaji wa gesi Tabata jijini Dar es Salaam. Anasema wanalazimika kupandisha bei ya bidhaa hiyo kwa madai kuwa imepanda wanakoinunua kwa wauzaji wa jumla.

“Unafikiri tunapenda kuuza hii bei dada yangu? Na sisi wale wanaotuletea kwa jumla wametupandishia. Kwa mfano, gesi ya ORYX mtungi wa kilo 15 tunauziwa 20,000 na wa kilo 30 tunauzwa Sh. 53,000 wakati gesi ya Taifa mtungi wa kilo 15 tunauziwa Sh. 17,000 na kilo 30 Sh. 58,000," anafafanua.

HALI ILIVYO KITAIFA

Kwenye maduka ya gesi yaliyoko Kwa Mrombo, Kata ya Muriet Wilaya ya Arusha, Nipashe ilimshuhudia Febronia James akinunua gesi ya Manjis kwa Sh. 54,000 kwa mtungi mkubwa huku udadisi ukibaini mtungi mdogo ulikuwa unauzwa kwa Sh. 21,500.

Mjini Njombe Nipashe ilishuhudia jana majira ya saa nane mchana mtungi kubwa wa kampuni ya ORYX ukibadilishwa kwa Sh. 55,000 huku baadhi ya maduka wakibadilisha kwa Sh. 58,000 wakati mtungi mdogo ukibadilishwa kwa Sh. 24,000.


 
"Kweli bei ya gesi imepanda ghafla, yaani imepandishwa kutoka Sh. 52,000 hadi Sh. 58,000, hii ni mbaya kwa kweli," alilalamika Aghata Kiyeyeu, mkazi wa mjini Njombe.

"Kwanza tuliamini gesi ndio mbadala wa mkaa lakini hali ni tofauti. Kupanda panda huku kwa bei ya gesi ni hatari kwa mazingira yetu kwa sababu watu watarudi kwenye mkaa tu," anaonya.

Mjini Moshi jana, mfanyabiashara Mwanajuma Hassan mwenye duka la gesi ya kupikia katika Mtaa wa Uswalini, aliiambia Nipashe mtungi mdogo wa gesi anauuza kwa bei ya jumla Sh. 48,000 na kujaza ni Sh. 22,000.

"Mtungi mkubwa bei ya kuuza ni Sh. 94,000 na kujaza ni Sh. 55,000 kwa Kampuni ya ORYX. Taifa na Orange, mdogo bei ya kuuza ni Sh. 39,000 na kujaza ni Sh. 20,000. Gesi ya Taifa bei ya kuuza ni Sh. 42,000 na kujaza ni Sh. 20,500.


Mjini Mwanza, Nipashe ilishuhudia jana majira ya saa 10 jioni mtungi mdogo wa kampuni ya ORYX ukibadilishwa kwa Sh. 24,000 na mkubwa Sh. 56,000 huku gesi ya Taifa ikibadilishwa kwa Sh. 22,000 kwa mtungi mdogo na Sh. 54,000 kwa mtungi mkubwa.

Jijini Dodoma, bei ya kujaza mtungi wa gesi aina ya ORXY ilikuwa Sh. 24,000 kwa mtungio mdogo kwenye maduka ya Mtaa wa Mtendeni huku mtungi mkubwa ukibadilishwa kwa Sh. 55,000 huku ile ya gesi ya Taifa ikibadilishwa kwa Sh. 22,500 na Sh. 53,000, mtawalia.

Miezi saba iliyopita serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), ilitoa zuio la kupandisha kiholela bei ya gesi ya kupikia.

Julai 17, mwaka jana, EWURA ilitangaza zuio hilo mpaka pale itakapopokea na kupitia mapendekezo ya hoja za uhalali wa kupandisha bei ya hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Edward Chibulunje, aliziagiza kampuni za gesi kuwasilisha EWURA maelezo ya uhalali wa kupandisha bei hizo kwa ajili ya uhakiki, huku akionya kampuni itakayoshindwa kufuata agizo la udhibiti kwamba hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.


from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/xU9OBra
via IFTTT

Comments

Popular posts from this blog

What Happened To Sarafina Skin? From Brown To White Skin – How Did It Happen? Explore The Real Story

MASHAIRI MATAMU YA MAPENZI