Wadau Waunga Mkono Kauli ya Profesa Mkumbo Kuhusu Kuufumua Mfumo wa Elimu



Dodoma/Dar. Wakati Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akieleza mkakati wa Serikali kuboresha elimu, wadau wa elimu wamesisitiza haja ya Serikali kuufumua mfumo wa elimu na kuusuka upya.

Kauli ya wadau hao imekuja baada ya Mbunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo ya kutaka mfumo wa elimu ufumulie kwa kuundwa kwa tume itakayochunguza na kuja na mapendekezo.

Akizungumza jana wakati wa hafla ya ugawaji wa kompyuta awamu ya tatu kwa vyuo vya ualimu chini ya Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Ualimu nchini (TESP) ulioanza kutekelezwa mwaka 2017/2018, Profesa Mkenda alisema suala la ubora wa elimu halihusu mitaala pekee bali kuna masuala mengine yanayochangia ikiwemo walimu na wakufunzi.

Katika hafla hiyo Serikali iligawa kompyuta 300 zilizogawiwa kwa vyuo 13 ambapo vyuo vinne vilipata kompyuta 30.


Vyuo tisa kompyuta 20 huku vyuo vyote 35 vikipatiwa kompyuta mpakato moja kwa ajili ya kusaidia idara zilizopo vyuoni.

“Unaweza ukawa na mitaala mizuri lakini walimu hawatoshi haisaidii hata hivyo tunavyoona wanafunzi wanaosoma shule binafsi na Serikali performance (matokeo) yao inatofautiana na sasa tunafanya utafiti,” alisema Profesa Mkenda.

Alisema ili kuinua ubora nchini inapaswa kuangalia mambo mbalimbali ikiwemo mitaala na jinsi ya kuandaa walimu wakufunzi wanaoweza kusaidia kuinua ubora wa elimu.


Alitaja mambo mengine ni miundombinu na vitendea kazi vya walimu ikiwemo na vitabu na maktaba iliyosheheni vitabu.

Alisema ukiangalia matokeo ya wanafunzi kwa mikoa, utagundua kuwa shule yenye walimu wachache ukilinganisha na idadi ya wanafunzi zimekuwa zikifanya vibaya kuliko zile zenye walimu wengi ukilinganisha na idadi ya wanafunzi.

Akielezea kuhusu mradi Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Calorine Nombo alisema mradi wa TESP unatekelezwa kwa ushirikiano kati Serikali ya Tanzania na Serikali ya Canada kupitia ubalozi wake nchini.

Wadau wataka mabadiliko

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, baadhi ya wadau wa elimu nchini wameungana na Profesa Kitila wakitaka mfumo wa elimu ubadilishwe.


Profesa wa Sayansi ya siasa ambaye pia ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu kishirikishi cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), Bernadeta Kilian alisema kuna haja ya kuboresha mfumo wa elimu nchini ili vijana wanaoishia njiani kimasomo na wale wanaofanikiwa kumaliza vyuo vya kati na vikuu waweze kujiajiri.

Alisema mfumo uboreshwe kwa kuongeza stadi zaidi na kuboresha mitaala ili mtoto anapomaliza hata kama hajawa na uwezo wa kuendelea mbele ile elimu aliyoipata imsaidie katika maisha yake.

Naye Kaimu Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) Kagera, Juliana Magesa alisema kuna ulazima kujizatiti na kutoa mafunzo yanayoendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia na kwamba lazima yafanyike maboresho ya mitaala.

Naye mdau wa elimu, Ezekiel Oluochi alisema kauli ya Profesa Kitila Mkumbo si ngeni na imekuwa ni wito wa wadau wengi.


Naye Mhadhiri wa Elimu wa Shule ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk George Kahangwa alisema licha ya wito wa kupitiwa upya kwa elimu kutolewa kwa muda mrefu, Serikali haijachukua hatua kutokana na mapitio madogo ya mara kwa mara yanayofanyika.

Mratibu wa kitaifa kutoka Mtandao wa Elimu Tanzani (Tenmet), Ochola Wayoga aliyesema jambo hilo si jipya kuzungumziwa juu ya mfumo wa elimu namna unasababisha changamoto kwa wahitimu katika ngazi mbalimbali.

Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Erasto Kano alisema asilimia kubwa watu wanapewa elimu ambayo imewafanya washindwe kujitegemea.


from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/znDhqb1
via IFTTT

Comments

Popular posts from this blog

What Happened To Sarafina Skin? From Brown To White Skin – How Did It Happen? Explore The Real Story

MASHAIRI MATAMU YA MAPENZI