Madiwani 41 Moshi Wamkataa Mkurugenzi wa Halmashauri Hiyo



Moshi. Madiwani 41 wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro wameandika barua ya kumkataa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Kastory Msigala wakimtuhumu kufanya maamuzi binafsi kupitisha baadhi ya miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo.

Madiwani hao walioandamana hadi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuwasilisha barua yao, wanalalamikia ukusanyaji wa mapato hafifu kutokana na utendaji usio shirikishi wa mkurugenzi huyo pamoja na utolewaji wa maamuzi ya utekelezaji wa miradi bila kushirikisha kamati ya fedha na baraza la madiwani.

Hatua hiyo imefikiwa ikiwa zimepita siku chache tangu madiwani wa Manispaa ya Moshi mkoani hapa, kupiga kura za kumkataa Meya wa Manispaa hiyo, Juma Raibu.

Akizungumza jana baada ya kikao cha madiwani kilichokaa ofisi za CCM wilayani Moshi, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Moris Makoi alisema tatizo hilo ni la muda mrefu na wamekuwa wakimlalamikia lakini hakuna mabadiliko, ndiyo maana wameamua kuandika barua hiyo. “Fedha za halmashauri zinapoletwa kutoka Serikali kuu kwa ajili ya maendeleo, mkurugenzi anatakiwa kutoa tangazo likieleza matumizi ya fedha hizo na kamati ya fedha ndiyo yenye mamlaka ya kuidhinisha manunuzi yote ya halmashauri kikanuni,” alisema.


Ujenzi Hospitali ya Wilaya

Katika hatua nyingine, Makoi alizungumzia changamoto ya Hospitali ya Wilaya, akisema Moshi kumekuwa na changamoto ya eneo na walitarajia wangekaa na mkurugenzi kukubaliana wajenge majengo ya ghorofa lakini imeonekana mkurugenzi alitaka lipatikane eneo la hekari 30 kwa ajili ya Hospitali hiyo.

“Jambo hilo lilisababisha Kamati ya Mipango na Fedha iitishe vigezo kutoka Wizara ya Afya, kujua ili eneo lijengwe hospitali ni nini ambacho kinahitajika, lakini tulipoletewa moja ya kigezo ilikiwa ni eneo husika kufikika na kata zote za halmashauri husika. Halmashauri hii ina majimbo mawili na kata 32.

Mwenyekiti huyo alieleza kuwa, awali mkurugenzi aliwaandikia madiwani wote barua kuwataka kutafuta eneo la kujenga hospitali hiyo na baadhi walileta lakini hakuyafuatilia na badala yake amekuwa akiwagawa na kutoa maamuzi binafsi.


Kwa upande wake Diwani wa Uru kusini, Wilhad Kitali alisema wamechaguliwa kutetea maslahi ya wananchi na inapofika mahali wanaona kasi ya ukusanyaji wa mapato inashuka ni lazima wapige kelele yaongezeke na fedha ipatikane kuwaletea maendeleo wananchi.

“Tumekutana madiwani katika ofisi za chama ili kujadili mwenendo mbovu wa halmashauri yetu, tumechaguliwa kuhakikisha tunapigania maslahi ya wananchi, leo tumefika hapa kuyazungumzia na tunaamini kwa kuwa CCM ni chama sikivu, malalamiko yetu yatafanyiwa kazi,” alisema.

Mkurugenzi, RAS wazungumza

Akijibu malalamiko hayo, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Kastory Msigala alisema Mwenyekiti wa Halmashauri ndiye msemaji mkuu na kama ana jambo atamwita mkurugenzi, likimshinda atalipeleka kwa mkuu wa wilaya au mkoa.

Hata hivyo alipoulizwa kuhusu madiwani hao kupeleka barua kwa mkuu wa mkoa, alisema anasubiri maelekezo ya mkoa.


Kwa upande wa Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro, Willy Machumu alithibitisha ofisi ya mkoa kupokea barua kutoka kwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Moshi Vijijini, aliyomuandikia Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, wakimtuhumu mkurugenzi wa halmashauri hiyo kukiuka taratibu na miongozo ya Serikali.

“Kwa utaratibu suala hili analishughulikia Mkuu wa Wilaya kwa kuwa ndiye mwenye wilaya husika. Sisi Mkoa tunasubiri vikao halali kati ya Mkuu wa Wilaya, mkurugenzi wa Halmashauri na mwenyekiti,” alisema Machumu.


Mwananchi


from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/KoaRFzQ
via IFTTT

Comments

Popular posts from this blog

What Happened To Sarafina Skin? From Brown To White Skin – How Did It Happen? Explore The Real Story

MASHAIRI MATAMU YA MAPENZI