Kicheko Tena Posho Watumishi wa Umma..Mama Anaupiga Mwingi Sana
BAADA ya kupandisha mishahara ya watumishi wa umma kwa asilimia 23, Rais Samia Suluhu Hassan amepeleka kicheko kingine kwao, safari hii akitoa kibali cha kurekebisha posho ya kujikimu ya safari za ndani ya nchi kwa watumishi wa umma na kiwango cha malipo ya kazi maalum (Extra Duty).
Kwa mujibu wa Ofisi ya Rais - Utumishi na Utawala Bora, utekelezaji wa kibali hicho umepangwa kuanza rasmi Julai Mosi, mwaka huu, yaani siku ya kwanza ya mwaka wa fedha 2022/23.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dk. Laurean Ndumbaro, alibainisha hayo jijini Dodoma jana wakati wa kikao kazi cha wakuu wa idara na vitengo vya utawala na usimamizi wa rasilimali watu katika utumishi wa umma chenye lengo la kutathmini utendaji kazi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Dk. Ndumbaro alisema kuwa kutokana na kibali hicho cha Rais, posho ya kujikimu ya safari za ndani ya nchi kwa watumishi wa umma kwa kiwango cha juu imepanda kutoka Sh. 120,000 hadi 250,000 na kiwango cha chini kutoka Sh. 80,000 hadi 100,000.
Aliongeza kuwa kiwango cha malipo ya kazi maalum (Extra Duty) kwa watumishi wa umma kimeongezeka kwa ngazi zote, ambapo kwa ngazi ya chini kimepanda kutoka Sh. 15,000 hadi 30,000, kwa ngazi ya kati kimeongezeka kutoka Sh. 20,000 hadi 40,000 na kwa ngazi ya juu kimeongezeka kutoka Sh. 30,000 hadi 60,000.
Dk. Ndumbaro alisisitiza kuwa viwango hivyo vipya vitalipwa na serikali kupitia bajeti iliyoidhinishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwaka wa fedha 2022/2023, hivyo taasisi zisiombe nyongeza ya bajeti ili kuwalipa viwango hivyo watumishi wake.
Kufuatia ongezeko hilo, Dk. Ndumbaro alitoa wito kwa watumishi wa umma wote nchini kufanya kazi kwa bidii, maarifa, weledi na nidhamu ya hali ya juu ili kuunga mkono kwa vitendo jitihada za Rais za kuboresha maslahi yao.
“Watumishi wa umma tuwajibike kwa hiari bila kushurutishwa, tuwe wabunifu zaidi ili kutoa mchango katika maendeleo ya Taifa na ustawi wa nchi kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kuhakikisha tunatatua kero zinazowakabili wananchi,” Dk. Ndumbaro alisisitiza.
Katibu Mkuu huyo pia alitoa wito kwa wakuu wa utumishi wa umma hususani walio katika halmashauri na taasisi zenye matawi, kuwatembelea watumishi wanaowasimamia kwenye maeneo yao ya kazi ili wabaini kero zinazowakabili na kuzitatua ili kuondoa shida ya watumishi kusafiri umbali mrefu kwenda makao makuu kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi kero zao.
“Mkiwafuata katika vituo vyao vya kazi, mtawasaidia kuwapunguzia gharama za kusafiri kwenda makao makuu ya wilaya, mkoa au makao makuu ya nchi kwa ajili ya kutatua changamoto zao kwani nyie viongozi mkiwatembelea serikali ndiyo itawagharamia,” alifafanua.
Rais Samia tangu aingie madarakani Machi 19 mwaka jana, amekuwa mstari wa mbele kuboresha stahiki za watumishi wa umma nchini ili kuwajengea ari na morali ya kutoa huduma bora kwa wananchi na hatimaye wananchi wajivunie uwapo wa serikali yao
from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/2WpAo6d
via IFTTT
Comments
Post a Comment