Balozi Sirro amshukuru Rais Samia, amzungumzia IGP Wambura

 



Butiama. Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Simon Sirro amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua katika wadhifa huo na kuahidi kwenda kutimiza majukumu yake kwa ufanisi.


Aidha, Balozi Sirro amewaomba Watanzania kumuombea Mkuu mpya wa Jeshi la Polisi (IGP), Camilius Wambura pamoja na timu yake ili waweze kutimiza majukumu yao vema kwa manufaa ya nchi.


Sirro ameyasema hayo leo Jumapili  Julai 24, 2022 kwenye misa ya shukrani aliyoifanya kijijini kwao katika Kanisa Katoliki Muriaza, Jimbo la Musoma Mkoa wa Mara.


Amefanya misa hiyo ikiwa ni siku takribani tano zimepita tangu Rais Samia kufanya mabadiliko ndani ya Jeshi la Polisi, Julai 19  2022 na kumbadilishia majukumu.


Katika mabadiliko hayo, Rais Samia alimteua Camilius Wambura aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kuwa IGP kuchukua nafasi ya Sirro ambaye aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zimbambwe.


IGP Wambura na Balozi Sirro kwa pamoja waliapishwa Julai 20, 2022 Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.


ADVERTISEMENT

Pia, Rais Samia alimteua Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma (RPC), Ramadhan Kingai kuwa DCI.


Akizungumza na waumini wa kanisa hilo, Balozi Sirro amesema Rais Samia amempa heshima kubwa hivyo hatamuangusha licha ya nafasi hiyo ya kidiplomasia kuwa ngeni kwake.


"Wenzetu wamezoea wanayafanya haya kidiplomasia, sasa mimi na hii sauti yangu ya uafande nitajitahidi kwendana nao naamini  nitaiwakilisha nchi yetu vizuri huko kwa uwezo wa Mungu na bahati nzuri nina uzoefu na hizi nchi za Kusini mwa Afrika," amesema Balozi Sirro


Amesema atatimiza wajibu wake kwa mujibu wa kiapo chake na maelekezo ya Rais hadi hapo itakapompendeza Rais kufanya uamuzi mwingine.


Balozi Sirro amesema baada ya kumaliza utumishi wake wa umma anatarajia kurudi kijijiji kwao Muriaza wilayani Butiama kuishi na wanakijiji wenzake.


Kuhusu viongozi wapya wa jeshi la polisi, Balozi Sirro amesema,"niwaombe Watanzania, mumuombee IGP wetu mpya Wambura pamoja na timu yake ili waweze kutimiza majukumu yao vema na kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa shwari."


"Mpeni ushirikiano wa kutosha ili tuweze kupata maendelo endelevu kwa maana bila amani hakuna maendeleo," amesema


Katika misa hiyo, Balozi Sirro pia amekabidhi misaada ya vitu mbalimbali kwa makundi maalum ya  Kanisa Katoliki majimbo ya Musoma na Bunda Mkoa wa Mara.


Amesema msaada huo umetolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kama zawadi kwa makundi hayo.


Zawadi hizo ni pamoja na mablakenti, taulo za kuogea na vyombo vya ndani ambapo wanufaika wa msaada huo ni pamoja na vituo vya watoto yatima, kwaya, ofisi za maaskofu na mapdri katika majimbo hayo.


Amesema Rais Samia anatamabua umuhimu wa madhehebu  ya dini katika kusimamia amani na usalama wa nchi.


Balozi huyo amesema wakati jeshi la polisi likifanya doria katika maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya usalama wa nchi, viongozi wa dini wao wamekuwa wakifanya doria ya kiimani hivyo kusaidia katika kuimarisha amani nchini.


Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Paroko msaidizi wa Parokia ya Butiama, Padri Philip Justine amemshukuru Rais kwa zawadi hizo ambazo zitasaidia katika kuongeza ari ya utendaji kazi kwa makundi hayo kanisani.


Padri Justine pia amemshukuru, Balozi Sirro kwa ushirikiano ambao amekuwa akiutoa kwa kanisa hilo kwa muda wote aliokuwa IGP huku akiwaomba waumini wa kanisa hilo kumuombea mafanikio balozi huyo katika majukumu yake mapya.


"Sote tunajua namna ambavyo umekuwa ukitoa kwaajili ya kazi ya Mungu, mfano hai ni hili kanisa uliloamua kujenga ili watu wa Mungu wapate eneo la kuabudia, haya yote unayafanya kwasababu ya utayari wako maana kutoa sio lazima mtu awe tajiri bali ni moyo wa mtu mwenyewe," amesema


Padri huyo amewaomba Watanzania kuiga moyo kama huo wa Balozi Sirro huku akiwataka kufanyakazi kwa bidii na kuepuka udanganyifu ambao umekuwa ukifanywa na baadhi ya watu ambao wamekuwa wakiwaaminisha Watanzania upo uwezekano wa kupata mali bila kufanya kazi.


"Wanakuja na kuwaambia fumba macho na upokee, hakuna kitu kama hicho, utapokea kutokana na namna unavyofanyakazi, badilikeni muombeni Mungu lakini mkumbuke kufanya kazi kama alivyoagiza katika maandiko matakatifu," amesema



from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/orMTy9b
via IFTTT

Comments

Popular posts from this blog

MASHAIRI MATAMU YA MAPENZI

What Happened To Sarafina Skin? From Brown To White Skin – How Did It Happen? Explore The Real Story