Mgonjwa aidai TMJ, Hindu Mandal fidia ya shilingi milioni 500

 


Dar es Salaam. Mfanyakazi wa Wizara ya Kilimo, Frorence Samwel anadai fidia ya Sh500 milioni Hospitali za TMJ na Hindu Mandal za jijini Dar es Salaam na daktari Moirice Mavura kwa kile anachodai kuwa ni uzembe katika kumtibu.


Pia amedai alipwe Sh53 milioni kwa ajili ya gharama mbalimbali, ikiwemo ya matibabu na usafiri.


Frorence amefungua kesi hiyo dhidi ya Dk Mavura pamoja na hospitali hizo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akidai kuwa hospitali hizo zilifanya uzembe alipokwenda kupata huduma ya matibabu.


Akitoa ushahidi wake katika kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Ramadhan Rugemalira huku akiongozwa na wakili wake Norbert Mlwale alidai kuwa Juni 27, 2018 alienda katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na alifanyiwa uchunguzi wa koo ndipo alielezwa amuone Dk Moirice Mavura.


Alidai baada ya kumuona Dk Mavura alimwelekeza kuwa aende katika hospitali ya Hindu Mandal kwa kuwa ina vifaa vya kisasa kwa ajili ya upasuaji na anafanya kazi katika hospitali hiyo.


Shahidi huyo aliieleza mahakama hiyo kuwa Julai 9, 2018 Dk Mavura alimfanyia upasuaji katika koo lake na alitoa sampuli za tezi la kushoto zikapelekwa katika hospitali ya TMJ kwa ajili ya uchunguzi.


Alidai baada ya kufanyiwa uchunguzi wa sampuli hiyo hospitali ya TMJ ilitoa ripoti yake ikidai kuwa alikuwa na ugonjwa wa Rapillary Carcinoma of Thyoid ambayo alikabidhiwa Dk Mavura.


Baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo Dk Mavura alimfanyia upasuaji wa pili na kuiondoa tezi iliyoambukizwa ugonjwa huo.


Anaeleza kuwa baada ya kufanyiwa upasuaji huo zilichukuliwa sampuli za tezi zenye ugonjwa huo na zilipelekwa katika Hospitali ya TMJ kwa ajili ya uchunguzi mwingine ambapo ripoti ilionyesha kuwa tezi hizo zipo sawa hazina ugonjwa wowote. Mdai huyo alipopewa majibu hayo alienda nayo hadi katika hospitali ya Hindu Mandal na alipofika aliambiwa akamuone daktari aliyetajwa kwa jina moja la Mavunda ambaye alimweleza amekutwa na kansa ya Thyroid hivyo anatakiwa aende katika hospitali ya Taasisi ya Saratani Ocean Road kwa ajili ya kuanza matibabu ya mionzi.


Anaeleza kuwa alipofika katika hospitali Ocean Road aliomba apimwe tena ili kujua kama ana tatizo hilo, ndipo walimwambia hawapimi upya kwa kuwa huwa wanategemea taarifa za mgonjwa kutoka hospitali husika.


“Nilipewa barua kutoka hospitali ya Hindu Mandal ili niende nayo hadi katika hospitali ya Ocean Road ili nianze matibabu ya mionzi,nilipofuatilia sikufanikiwa nikawa ninazunguushwa huku afya yangu ikiendelea kudhoofika huku ngozi yangu ikisinyaa kama mzee huku nywele zangu zikinyonyoka,” alidai Frorence.


Alidai baada ya kuikosa huduma ya mionzi alichukua uamuzi wa kukopa fedha benki na kuuza kiwanja chake huku ndugu zake wakimchangia fedha ili aweze kwenda hospitali ya Apollo iliyopo nchini India kwa ajili ya uchunguzi zaidi.


Baada ya kupata fedha hizo akaenda katika hospitali ya Hindu Mandal ili apewe barua pamoja na sampuli za tezi hizo aweze kwenda nazo katika hospitali ya Apollo kwa ajili ya uchunguzi zaidi.


“Nilipewa sampuli ambazo zilifungwa kama nilivyokabidhiwa, nilizipeleka moja kwa moja hadi katika hospitali ya Apollo iliyopo nchini India, zilifanyiwa uchunguzi na ilionekana sikuwa na kansa ya Thyoid,” alidai Frolence.


Anasema madaktari wa hospitali ya Apollo walibaini tezi yote ya Thyoid ya kushoto inayosaidia kutengeneza homoni imeondolewa wakati alipofanyiwa upasuaji huo katika hospitali ya Hindu Mandal, jambo ambalo limemsababishia ngozi yake kusinyaa na nywele kunyonyoka.


“Mimi nilikuwa najua nimefanyiwa upasuaji wa goita na sikuwahi kuambiwa na hospitali ya Hindu Mandal kama wamenitoa tezi, nimekuja kujua baada ya kuelezwa na hospitali ya Apollo ya nchini India kuwa kinachonisumbua ni upungufu wa homoni na siyo kansa.


Anadai hospitali ya Apollo ilimuandikia dawa za kuongeza homoni ambapo alielezwa katika maisha yake yote atakuwa anatumia dawa hizo, hatakiwi kuacha na asipofuata masharti hayo ngozi yake itasinyaa na nywele zitanyonyoka.


Baada ya maelezo hayo, Hakimu Rugemarila aliahirisha shauri hilo hadi Septemba 13,,2022 kwa ajili ya kuendelea na ushahidi wa upande wa mdai.


Source: Mwananchi, July 24



from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/cgL27MV
via IFTTT

Comments

Popular posts from this blog

What Happened To Sarafina Skin? From Brown To White Skin – How Did It Happen? Explore The Real Story

MASHAIRI MATAMU YA MAPENZI