Mchezaji Akpan Apindua Meza Simba..Sasa Kubakia Kikosini
MABOSI wa Simba walipanga kabla ya dirisha la usajili kufungwa Agosti 31, kushusha kiungo mmoja mkabaji ili kuchukua nafasi ya Victor Akpan ambaye Kocha Zoran Maki alimkataa tangu timu ikiwa kambini nchini Misri, lakini Mnigeria huyo amepindua meza kiaina, kwani sasa atasalia kikosini.
Ipo hivi. Kocha Zoran alipanga kumtoa kwa mkopo Akpan na wachezaji wengine kadhaa akiwamo Nassor Kapama, kisha akataka aletewe kiungo mkabaji mpya na fasta mabosi wa Simba walimtuma mmoja wa vigogo wa klabu hiyo kwenda kumalizana na viungo wawili wote kutoka Nigeria.
Viungo waliokuwa kwenye rada za Simba ni Afeez Nosiri kutoka Kwara United na Morice Chukwu wa Rivers United, lakini kigogo aliyekwenda kuwafuata alikutana na kigingi cha mikataba waliyonayo, hivyo dili la wachezaji hao kufa rasmi na kutoa nafuu kwa Akpan na wenzake.
Taarifa hiyo ya dili la kina Chukwu kuzikwa rasmi, imemfanya Kocha Zoran naye kutoa msimamo wa kutotaka mchezaji hata mmoja kati ya waliopo kikosini kwa sasa kutoka na kama kutakuwa na uamuzi mwingine basi utafanywa kwenye dirisha dogo.
Kocha huyo alisema kutokana na utulivu uliopo katika kikosi chake pamoja na uhitaji wa kila mchezaji hakuna atakayeondoka katika dirisha hili kwani wote watasalia kwenye kikosi ili kuendeleza moto walioanza nao katika Ligi Kuu Bara iliyosimama kwa muda.
Zoran alisema kulikuwa na mpango wa kuboresha kikosi kabla ya dirisha la usajili kufungwa kuingiza mchezaji mpya eneo la kiungo, ila kutokana na changamoto zilizo nje ya uwezo wao jambo hilo halipo tena.
“Wachezaji wote wapya na wale waliokuwepo kwenye kikosi msimu uliopita hakuna hata mmoja atakayeondoka. Wote nitabaki nao kwa ajili ya kuhakikisha tunapambana na kupata matokeo mazuri katika kila mechi kwenye mashindano ya ndani na yale ya CAF,” alisema Zoran.
“Wachezaji wote ambao hawapo katika majukumu ya timu za taifa nitakwenda nao Sudan katika michezo miwili ya kirafiki na tutatumia mwaliko huo kama sehemu ya maandalizi kabla ya michezo ya mashindano.”
Awali, Simba ilipanga kuwa kama ingepata kiungo mmoja kati ya Nosiru au Chukwu, basi Akpan aliyesajiliwa kutoka Coastal Union angetolewa kwa mkopo kutokana na kushindwa kulivutia benchi la ufundi.
Akizungumza na Mwanaspoti juzi Jumatano, Akpan alisema alikuwa anaona tu taarifa hizo katika mitandao ya kijamii na hakupewa taarifa yoyote rasmi kutoka kwa viongozi ndio maana alikuwa anaendelea na ratiba ya timu kila siku kama ilivyopangwa.
“Nipo kambini kwa ajili ya mazoezi jioni na nitakuwepo kwenye orodha ya wachezaji ambao tunakwenda kucheza mechi mbili za kirafiki Sudan,” alisema Akpan.
from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/VGxQbYB
via IFTTT
Comments
Post a Comment