Washukiwa watano wa ujambazi wauawa, saba watoroka Iringa
Ramani ya Mji wa Mafinga
WATU watano wanaodhaniwa kuwa ni majambazi kati ya 12 wamefariki dunia baada ya kujeruhiwa katika majibizano ya risasi na Polisi wakati wakijaribu kufanya uhalifu katika kiwanda cha Daazhong kinachomilikiwa na wawekezaji kutoka China kilichopo katika kijiji cha Changarawe, wilayani Mufindi mkoani Iringa.
Akizungumza na wanahabari katika eneo la tukio leo Ijumaa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amesema washukiwa hao walifariki wakati wakikimbizwa Hospitali ya Mji wa Mafinga kutokana na majeruhi ya risasi waliyoyapata.
Alisema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo, Septemba 30, majira ya saa 8.00 usiku na washukiwa wengine saba walitokomea kusikojulikana.
“Mnamo Septemba 29, mwaka huu ,Jeshi la Polisi mkoa wa Iringa lilipokea taarifa za kuwepo kwa majambazi 12 waliopanga kufanya uhalifu katika kiwanda hicho,” alisema.
Baada ya kupokea taarifa hiyo alisema, Jeshi liliweka mtego kwa ajili ya kuwakamata wahalifu hao, waliovamia katika kiwanda hicho usiku wa kuamkia leo, Septemba 30.
“Timu ya askari wetu waliwaamuru wahalifu hao wajisalimishe lakini walikaidi amri hiyo na kuanza kuwarushia askari risasi,” alisema.
“Katika tukio hilo tulifanikiwa pia kupata silaha mbili, moja ikiwa ni aina ya Shotgun na nyingine ikiwa ni pump action. Pia yalipatikana mabegi mawili ya mgongoni ambalo moja kati yake lilikuwa na sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWT) na risasi 13 za shotgun,” alisema.
Katika begi jingine alisema kulikuwa na sare za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), jaketi moja la mtumba na kitambaa vilivyofanana na kombati ya jeshi, shoka moja na nyundo moja.
“Pia katika moja ya mabegi hayo kulikuwa na line 12 za Tigo, Airtel 25 na Vodacom saba,” alisema.
Alisema jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka wahalifu wengine waliohusiska katika tukio hilo na akatoa wito kwa watu wengine wanaopanga kufanya uhalifu waache na kusalimisha silaha zao.
“Aidha tunaendelea kuwashukuru wananchi wa mkoa wa Iringa kwa kuendelea kutupa taarifa zinazotusaidia kukabiliana na uhalifu,” alisema.
from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/y3mMUwb
via IFTTT
Comments
Post a Comment