Yanga yang’oa fundi Mazembe




KIKOSI cha Yanga kinaendelea kupiga tizi jijini Dar es Salaam kujiandaa na mechi zijazo za Ligi Kuu Bara na zile za Ligi ya Mabingwa Afrika zitakazopigwa mwezi ujao, lakini mabosi wa klabu hiyo wamefanya jambo moja la akili kwa kumng’oa fundi mmoja kutoka TP Mazembe ya DR Congo.

Mabosi hao wa Yanga wamemleta aliyewahi kuwa kigogo wa TP Mazembe na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Klabu ya Power Dynamos ya Zambia pamoja na Chama cha Soka cha Zambia (FAZ), Andre Mtine ambaye tayari yupo jijini Dar es Salaam na kanaswa ‘live’ na Mwanaspoti.

Katika toleo la Mwanaspoti la Septemba 4 mwaka huu, tuliripoti juu ya mpango wa Yanga kumleta mtendaji mkuu (CEO) Mzambia kutoka TP Mazembe na juzi lilimnasa jamaa huyo akitinga hoteli aliyofikia baada ya kuletwa na mabosi wa Jangwani, huku kukiwa na taarifa Mtine ndiye anayekuwa CEO mpya.

Ingawa hakuna kiongozi yeyote wa Yanga aliyepatikana kuweka bayana ya huyu Mtine, lakini habari za kuaminika kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema Mzambia huyo tayari ameshakula shavu baada ya kukubaliana na kimaslahi na wanene wa Yanga akipewa mkataba wa ajira kama mtendaji mkuu akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Msauzi Senzo Mazingiza aliyemaliza mkataba wake Jangwani.


Mara baada ya Senzo kuondoka Agosti, mwaka huu, nafasi yake imekuwa ikikaimiwa na Simon Patrick, hivyo kuja kwa Mtine imemaliza juu ya tetesi zilizokuwapo kwani inaelezwa tayari ameanza kazi akisubiri kutambulishwa rasmi na mabosi wa klabu hiyo inayoongoza katika msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa sasa.

Mtine anakumbukwa na Wazambia akiwa mtendaji mkuu wa Nkana miaka ya 1980 na kuifanya iwe tishio Afrika kabla ya mwaka 2000-2004 alipotinga Power Dynamos ambayo ni klabu pinzani ya Nkana na kuifanya ishinde ubingwa wa Ligi Kuu ya Zambia na pia kubeba mataji matano ya ndani.

Pia aliwahi kuitumikia kamati ya fedha ya Shirikisho la Soka Afrika kabla ya kuchukuliwa na TP Mazembe na kuitumikia kwa nafasi mbalimbali ikiwamo kuwa msaka vipaji ‘skauti’ wa klabu hiyo kwa Zambia na kuipelekea timu timu nyota walioipa mafanikio makubwa barani Afrika na duniani ikiwamo kufika fainali ya Klabu Bingwa ya Dunia 2010 na kuvaana na Inter Milan ya Jose Mourinho ambapo ililala mabao 3-0.

Mabosi wa Yanga wameamua kumbeba mwamba huyo kutokana na mafanikio aliyonayo katika klabu alizozitumikia kwa nafasi mbalimbali ikiwamo mhasibu na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya FAZ, japo aliwahi kuingia matatani na kufungiwa maisha 2014 na shirikisho hilo kwa tuhuma za kuchafua jina la soka la kuzuia nyota watatu wa TP Mazembe kujiunga na timu ya taifa kwa madai ni majeruhi wakati haikuwa hivyo. Hata hivyo alikata rufaa na kufutiwa kifungo hicho.

Inaelezwa Mtine ni mtu wa mipango na taaluma yake ya kiuchumi na kujua soka kwa kiwango cha juu akirithi kipaji cha baba yake Tom Mtine aliyewahi kuwa Rais wa FAZ na mjumbe wa CAF, imewavutia Yanga iliyopo kwenye mchakato wa kuendeshwa kwa mfumo wa hisa baada ya mabadiliko yaliyofanywa na kusimamiwa na Senzo aliyekuwa amejiunga na Yanga akitokea Simba.

Senzo pia ndiye aliyehusika kwenye mabadiliko ya mfumo wa hisa kwa klabu ya Simba kabla ya kufanya mambo ndani ya Yanga akishirikiana na matajiri wa klabu hiyo GSM walioendesha mchakato ikiwa ni kubadili katiba iliyopitishwa na kuruhusu sasa klabu kuongozwa na rais badala ya mwenyekiti.

Mwanaspoti




from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/b4MYrF8
via IFTTT

Comments

Popular posts from this blog

MASHAIRI MATAMU YA MAPENZI

What Happened To Sarafina Skin? From Brown To White Skin – How Did It Happen? Explore The Real Story