Wamiliki wa Shule Wamvaa DR Mkenda Sakata la Kuifungia Shule ya Chalinze Modern




Dar es Salaam. Umoja wa Wamiliki na Maneneja wa shule binafsi Tanzania (Tamongosco), wameingilia kati suala la kufungiwa kwa Shule ya Chalinze Modern Islamic kuwa kituo cha mitihani wakitaka uamuzi huo utenguliwe.

Tamongosco wamejitosa katika sakata hilo ikiwa ni siku chache tangu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda kutangaza uamuzi huo baada ya kubainika watahiniwa saba walibadilishiwa namba za mtihani katika kituo cha mtihani chenye usajili na namba PS1408009.

Oktoba 25 mwaka huu, waziri huyo alichukua uamuzi huo kufutia malalamiko ya mtahiniwa Iptisam Suleiman Slim wa kituo cha mtihani cha shule hiyo kueleza alibadilishiwa namba yake ya mtihani wakati akifanya mtihani wa taifa wa darasa la saba uliofanyika Oktoba 5 na 6 mwaka huu.

Uchunguzi wa timu iliyoundwa ilibaini wanafunzi saba akiwemo Iptasam walibadilishiwa namba katika baadhi ya masomo yao hivyo Waziri Mkenda aliagiza kuchukuliwa hatua kwa watumishi wa shule waliohusika na kadhia hiyo pamoja na kukifungia kuwa kituo cha mitihani kwa muda usiojulikana.

Juzi, Mwenyekiti wa Tamongosco, Leonard Mao, alisema licha ya kupongeza hatua ya haraka iliyochukuliwa na Serikali kufanya uchunguzi ili kuthibitisha au kukanusha taarifa ambayo mtahiniwa husika aliitoa kupitia mitandao ya kijamii, umoja huo haujaridhishwa na hatua ya kufungiwa kwa kituo hicho.

Mao aliomba Serikali kuangalia namna sekta zingine zinavyosimamiwa na njia hizo zitumike hata kwenye elimu.

Alisema kosa linapofanyika, adhabu iende kwa mtu husika aliyetenda kosa na sio kuwaadhibu wasio na hatia.

Katika kuwasilisha malalamiko yao, tayari umoja huo umeshaandika barua kwa Waziri Mkenda kueleza kutoridhishwa kwao na uamuzi huo wa kukifungia kituo hicho kwani athari yake ni kubwa si tu wa wanafunzi walio madarasa ya chini, bali hata kwa wazazi wanaolazimika kuhangaika kutafuta shule nyingine kwa ajili ya watoto wao na mmiliki wa shule ambaye hakuhusika kwa namna yoyote katika kosa lililofanyika.


“Tumebaini utata katika maeneo kadhaaa ikiwemo mazingira ya wanafunzi kupewa namba tofauti na zile zilizo kwenye mfumo wa Necta, matokeo ya uchunguzi na hatua ambazo Serikali imezichukua,” alisema Mao na kuongeza:

“Kwa lengo la kuona kwamba haki inatendeka na bila kuathiri dhana nzima ya kuhakikisha elimu bora inaendelea kutolewa kwa wote, tumeona ni vema kuiarifu wizara kuhusu maoni yake ili utata huo uondolewe kwa manufaa ya umma.”

Waziri ajibu

Gazeti hili lilimtafuta Waziri Mkenda baada ya kilichoelezwa na umoja huo; naye alisema amepokea barua ya Tamongosco na anayafanyia kazi mapendekezo waliyotoa.

Kuhusu kufungwa kwa shule hiyo alisema, uamuzi aliotoa ni kuifungia shule kuwa kituo cha kufanyia mitihani na sio kama shule, hivyo wanafunzi wataendelea kusoma, ila mitihani watatakiwa kufanya katika vituo vingine.

“Mapendekezo yao tumeyapokea, tutayafanyia kazi. Kuhusu hiyo kanuni inayozungumziwa (ya kufungiwa kituo) iko kwa ajili ya kudhibiti udanganyifu kwenye mitihani. Halafu niliweke wazi hili shule haijafungwa kwa watoto kusoma; imefungwa kuwa kituo cha mtihani, na lengo ni kuwafanya hata wenye shule wachukizwe na vitendo vya watu wanaojaribu kuchezea mitihani,” alisema Profesa Mkenda.



from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/FAxE7KC
via IFTTT

Comments

Popular posts from this blog

MASHAIRI MATAMU YA MAPENZI

What Happened To Sarafina Skin? From Brown To White Skin – How Did It Happen? Explore The Real Story