Hatari Mikopo ‘Kausha Damu’
Dar es Salaam. Ongezeko la taasisi zinazotoa mikopo ‘chap chap’ yenye riba kubwa na kugeuka machungu kwa wakopaji, imeelezwa kuwa chanzo cha msongo wa mawazo kwa mdaiwa, kufariki kwa shinikizo la damu au kukimbia kusikojulikana.
Mikopo hiyo iliyopachikwa jina la ‘kausha damu’ kutokana na maumivu wanayopata wakopaji wakati wa kurejesha fedha, baadhi ya taasisi zimekuwa zikitoa masharti magumu, ikiwamo kutaifisha mali zikiwemo nyumba, magari na samani za ndani endapo mhusika atashindwa kulipa kwa wakati.
Uchunguzi uliofanywa na Mwanachi umebaini kuwa wanaoshindwa kurejesha mikopo kwa wakati, wamejikuta mali walizoweka kama dhamana zikitaifishwa na kuuzwa katika mazingira yasiyotoa fursa kuweza kupinga uuzwaji wa mali zao hizo.
ALSO READ
Mtoto anapenda soka? Njia sahihi za kumlinda
Makala 6 hours ago
Kampeni zapamba moto uchaguzi UWT
SIASA 6 hours ago
Taasisi ya mikopo yaeleza
Mtendaji wa Kampuni ya Jojo Microfinance iliyopo Pugu Bombani, Alice Zebedayo alisema unapotaka kuchukua mkopo huo lazima ununue fomu kwa Sh5,000 kwanza ili usajiliwe kisha hatua zifuate.
Akizungumza na Mwananchi, Alice alisema fomu hiyo ikisharudishwa anayekopa anatakiwa atoe Sh5,000 nyingine ili viongozi wa kampuni hiyo wanapokwenda kumtembelea nyumbani kwake waangalie samani za ndani vitakavyowekwa dhamana ya mkopo husika.
“Kama ukichukua Sh100,000 utapewa Sh90,000 baada ya kukatwa Sh5,000 ya fomu na Sh5,000 ya kukutembelea nyumbani kwako ili kuangalia vitu vitakavyowekwa dhamana; halafu riba ya mkopo ni Sh30,000, hivyo unatakiwa ulipe Sh130,000 kwa mwezi mmoja,” alisema Alice.
Akifafanua namna ya kulipa, alisema mtu anapochukua Sh100,000 kila siku anatakiwa kulipa Sh4,300, “na ndani ya mwezi mmoja awe amemaliza na akikosa siku moja kulipa faini ya Sh2000 itamhusu kwa kukiuka.
“Kwa anayechukua Sh50,000 atalipa Sh65,000 na riba na kila siku anatakiwa atoe rejesho la Sh2,200 na akikosa siku moja anatakiwa alipe faini ya Sh2,000 na inategemea, siku zikiwa nyingi na hela hiyo inazidi kuwa kubwa.”
Alisema ukiwa mlipaji mzuri wa marejesho hayo hata kama utahitaji kukopa Sh1 milioni unapewa, lakini riba yake ni asilimia 30. “Tutakubaliana kila siku utoe marejesho shilingi ngapi ndani ya mwezi mmoja, ni makubaliano.”
Kanuni ya mkopo ikoje?
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili jijini Dar es Salaam, umebaini kuwepo kwa kasoro nyingi katika baadhi ya wakopeshaji, ujanjaujanja wa kucheza na maneno ya mkataba huku wengi wao wakiweka riba kubwa zinazotakiwa kulipwa ndani ya kipindi kifupi.
Pia, umebaini wapo watu binafsi wanatoza riba hadi asilimia 30 kwenye mikopo hiyo kwa mwezi, vinginevyo mkopaji hupigwa faini kabla ya adhabu nyingine.
Kwa mujibu wa kanuni za mkopo midogo ya mwaka 2019 kifungu cha 37, kinamtaka mkopeshaji kutunga sera ya mikopo ikieleza mchakato wa ukopeshaji na nyaraka, masharti ya kukopa, aina ya mikopo na dhamana inayokubalika. Mengine ni pamoja na ukomo wa mkopo kwa kila mkopaji, vipindi vya mkopo na masharti kama riba, ada na changizo na malipo ya mara kwa mara.
Pia, sera hiyo inatakiwa kuonyesha mchakato wa kuidhinisha mkopo, uwezo wa mkopaji, ufuatiliaji na uthaminishaji na kipindi cha neema kama itawezekana.
Wanachosema wakopaji
Waathirika wakubwa wa mkopo huo ni wanawake ambao wamekuwa wakiishia kufilisiwa mali zikiwemo samani za ndani kama vitanda, majokofu, luninga pamoja na vyombo vya kupikia.
Mfanyabiashara katika Soko la Kitunda, Salama Hussein alisema yeye ni mmoja wa walioathirika na mkopo wa ‘kausha damu’ baada ya kukopa Sh200,000 ambayo riba yake ni Sh60,000 ndani ya mwezi mmoja.
Salama alisema kabla ya kupewa mkopo huo aliotakiwa kurejesha jumla ya Sh260,000, alinunua fomu ya kujiunga Sh10,000 na alitakiwa atoe Sh5,000 wakati alipotembelewa nyumbani kwake na maofisa wanaotoa mkopo ili waangalie vitu vya ndani vitakavyowekwa kama dhamana.
Alisema kutokana na shida aliyokuwa nayo alilazimika kuchukua Sh185,000 baada ya Sh15,000 kukatwa kwenye fomu na kutembelewa nyumbani.
Salama alisema kila siku alikuwa anarejesha Sh8,000, wakati mwingine alikuwa anakosa hela na kutakiwa kulipa faini ya Sh2,000 kwa siku ambayo hapeleki rejesho.
“Kutokana na ugumu wa maisha, biashara yangu ilikufa kwa sababu mkopo niliochukua umerudi kwa walionikopesha, kila siku nilikuwa natoa Sh8,000 bado sijapigwa faini ya Sh2,000 nikikosa kurejesha,” alisema alisema Salama.
“Kuna siku moja nilikuwa nalaza hadi siku tatu nalipa Sh6,000, kutokana na msingi wangu kuwa mdogo ulikufa, hela ya matumizi nayo nilikuwa nachukua kwenye biashara yangu.”
Mfanyabiashara wa Soko la Kigogo, Aisha Salehe alisema alikopa Sh50,000 kwenye taasisi moja ya kukopesha fedha kwa lengo la kuongezea mtaji katika biashara yake, lakini matokeo yake alichukuliwa godoro na sasa analala chini.
Aisha alisema aliambiwa atoe Sh5,000 kwa ajili ya fomu, Sh5,000 za kutembelewa na maofisa wanaotoa mkopo na amana ya mkopo alitoa Sh10,000.
Alisema riba aliyotakiwa kutoa ni Sh15,000, jumla ya fedha anazotakiwa kurejeshwa kwa mwezi Sh65,000 na kila siku alikuwa anatakiwa kutoa Sh2,200 kwa ajili ya rejesho.
“Ukichukua Sh200,000 lazima ulipe pamoja na riba, kila siku ‘kausha damu’ unatakiwa upeleke Sh4,300 na ukituma lazima utume na ya kutolea, usipotoa kwa siku moja faini yake ni Sh2,000 na hela yenyewe wanakupa Sh175,000 baada ya kukata fedha ya fomu, amana na wanapokutembelea nyumbani kwako.”
Aisha alisema kuna wengine wanachukua hadi Sh1 milioni, riba ya mkopo huo ni asilimia 30 nayo unalipa ndani ya mwezi mmoja, kila siku unatakiwa utoe Sh40,000 kama rejesho na usipotoa kwa siku faini yake ni Sh20,000.
Serikali ya mtaa yanena
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Pugu Bombani ambako baadhi ya wananchi wamelalamikia mikopo hiyo, Amanzi Bundala alisema ‘kausha damu’ katika mtaa wake vikundi vinavyokopesha vipo vingi na vimekuwa kero kwa wananchi wake.
“Mtu akichukua Sh50,000 kuna mambo mawili, la kwanza analipa kila siku Sh2,500 na ya pili wanatoka kwenye uhalisia wa biashara, kisha zinakuwa ngumu; hebu fikiria leo hii mtu akichukua Sh50,000 kwa ajili ya kujikwamua kibiashara haiendi kama alivyotarajia, matokeo yake vyote vinachukuliwa na huyo mkopeshaji,” alisema Bundala.
Hata hivyo, alisema amebaini wanaotoa mikopo hiyo baadhi yao hawana vibali, jambo ambalo ni tatizo kwa kuwa nchi inakosa mapato na Serikali ya mtaa huo hawapati chochote.
Machungu mengine ya mkopo huo yanasimuliwa na mkazi wa Tabata, Ibrahim Abdalla kwa kusema, “mimi nilikopa Sh500,000 kwa mtu binafsi na kila Sh100,000 riba ni Sh30,000 kwa mwezi, aise! Nilikuwa na shida, lakini maumivu yake ni makali sana.
“Kutokana na riba kuwa kubwa, nilijikuta deni linafika zaidi ya Sh1 milioni, kuna nyakati nilishindwa kulipa mkopo na kubaki kulipa riba tu, kwa hiyo hii ni changamoto sana ya mikopo umiza,” alisema Abdalla.
Mkopaji, mkopeshaji nani tatizo?
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kutetea Haki za Wanawake (HDO), Prisca Ngaeshemi alisema wanaochukua mkopo wa ‘kausha damu’ ni wajasiriamali wa chini, wakiwamo mamalishe, wauza vitumbua na mbogamboga.
Prisca alisema wanawake hao wanapochukua mkopo urejeshaji wake ni shida, huku akitolea mfano anayechukua Sh200,000 kila siku anatakiwa atoe Sh8,000, “biashara gani inayomfanya apate faida ya kupata hela hiyo.”
Alisema matokeo yake mtaji unakufa kwa sababu hela hiyo hiyo inampasa atoe ya matumizi ya nyumbani na nyingine kwa jili ya marejesho ya kila siku.
Hata hivyo, Wakili John Seka alipoulizwa kuhusu utendaji wa kampuni hizo, alisema kuna faida ya kila mkopo, huku akieleza wanaokopa huko na kutatua shida zao, ndiyo wanajua umuhimu wake na huenda tatizo likawa ni wateja.
Alisema kabla ya kuangalia uvunjaji wa sheria ni vyema kuangalia hatari kiasi gani wanabeba watu hawa wanaokopesha mikopo hiyo.
“Licha ya mikopo yao kutoka ndani ya muda mfupi, lakini (mkopaji) hana uhakika kama wanatumia muda wa kutosha kufanya ufuatiliaji wa mtu wanayemkopesha kama inavyofanywa na benki,”alisema wakili huyo.
“Benki ukiomba mkopo watakufanyia ufuatiliaji wa vitu vingi ili kujiridhisha kuwa wanayekwenda kumpa mkopo wao atarudisha, lakini hawa wanaweza kukupatia mkopo kwa kutumia kadi ya gari, hawakagui gari ni nzima kiasi gani kama inaweza warudishia pesa zao ila wanakuamini.”
Madalali wafunguka
Potess Moshi kutoka Mem Auctionineer and General Broker Limited alisema kuna tatizo la watu wanaochukua mikopo kutojua wanaenda kufanya nini na kama walikuwa na wazo, tayari hubadilika baada ya kupata fedha.
“Mtu anachukua mkopo anafanya rejesho moja halafu haonekani, sasa hatujui kama ni kwa sababu ya riba kubwa au biashara kuanguka,” alisema Moshi.
Alisema wengine hadi wanapewa mkopo wanakuwa na hela pungufu tofauti na iliyopo kwenye fomu kwa sababu wanatoa rushwa ili waonekane wana vigezo.
Dalali huyo alisema hali hiyo imewafanya kwa mwaka kuwa na uwezo wa kuletewa hadi dhamana 50 za wateja ili ziwekwe sokoni huku akieleza wakati mwingine zinashindwa kuuzika kutokana na uthamini wake kuwa tofauti.
“Kuna dhamana nyingine zinakuja zikiwa zimethaminiwa kwa gharama kubwa, lakini mteja akija kuangalia thamani yake haiendani hivyo haziuziki,” alisema Moshi.
Pia, alisema kwa mwaka unaweza kupata hata dhamana za watu 50, huku akieleza kuwa wingi wa madalali umechangia kazi kugawanywa.
Scholastica Kevela, ambaye ni Mkurugenzi wa Yono Auction Mart alisema kwa mwaka wanaletewa zaidi ya mali 100 za wateja ambao wameshindwa kulipa madeni yao kutoka taasisi za kifedha na Vyama vya Kuweka Akiba na Kukopa (Saccos).
“Kati ya hizo ndani yake ndiyo kuna nyumba, viwanja, kitu chochote alichoweka dhamana mteja,” alisema Scholastica.
Mkurugenzi wa Cops Auction Marts, Mohammed Mmanga alisema kwa miezi miwili wanaweza kupata hata nyumba 30 ambazo ni dhamana kutoka kwa taasisi za kifedha, ikiwamo benki mbalimbali.
Alisema kati ya nyumba hizo wanaweza wakauza au wasiuze hata moja kutokana na wateja kudanganya thamani ya fedha.
“Shida ni kuwa wakopaji wengi huwa hawasomi mikataba kwa sababu wana uhitaji wa hela, wakichukua mikopo wanafanyia kazi tofauti na walichoomba,” alisema Mmanga.
“Riba kubwa zipo kwa baadhi ya taasisi ila sio zote, wakopaji wanapaswa kujua wanakopa ili wafanye nini na wafanye kile walichokusudia, siyo kuchukua mkopo unaenda kumnunulia mke wako Iphone ya Sh3 milioni.”
Alipotafutwa Katibu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Twaha Mwakioja alisema kwa mujibu wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018 na Kanuni Zake za Mwaka 2019, biashara ya huduma ndogo za Fedha inasimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na wameweka ukomo wa riba, kiwango ambacho hakizidi asilimia 3.5 kwa mwezi.
“Kwa mujibu wa kanuni ya huduma ndogo za Fedha (majukumu ya waziri) ya mwaka 2019, wizara imeteua waratibu 212 kila mkoa na halmashauri, hivyo tunaomba nyaraka za mkopaji ikiwa ni mkataba wa mkopo ili tuweze kufuatilia na kuchukua hatua,” alisema Mwakioja.
Kauli ya BoT
Kwa mujibu wa taarifa ya BoT, wananchi wametakiwa kuepuka kukopa au kufanya biashara na taasisi, kampuni, mtu na watu binafsi ambao hawana leseni.
Hiyo ni baada ya kubaini kuna taasisi, kampuni na watu binafsi wanaojihusisha na biashara ya kutoa mikopo bila leseni, jambo ambalo ni kinyume na Kifungu cha 16(1) cha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018.
“Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuutaarifu umma kuwa taasisi, kampuni na mtu binafsi wasio na leseni husika hawaruhusiwi kufanya biashara ya kukopesha,” inaeleza taarifa ya BoT.
“Kwa mujibu wa Kifungu cha 16(2)(a) cha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018, hatua zitakazochukuliwa kwa ukiukaji wa sheria hiyo ni pamoja na faini isiyopungua Sh20 milioni au kifungo kwa muda usiopungua miaka miwili.
“Orodha ya taasisi, kampuni na watu binafsi wenye leseni za biashara ya kukopesha zilizotolewa na Benki Kuu ya Tanzania inapatikana kwenye tovuti ya Benki Kuu ambayo ni www.bot.go.tz.”
Mwananchi
from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/7SoclKr
via IFTTT
Comments
Post a Comment