Mhadhiri SAUT adaiwa kuuawa kwa kunyongwa




Mwanza. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT) Mwanza, Hamida Mussa maarufu 'Mama Mwakitosi' (64) anadaiwa kuuawa kwa kunyongwa na mtandio shingoni na mfanyakazi wa ndani ambaye alitokomea kusikojulikana baada ya tukio hilo.

Mwili wa Hamida ulikutwa jana Jumanne Novemba 29, 2022 nyumbani kwake Mtaa wa Buzuruga Mashariki wilayani Ilemela mkoani Mwanza ukiwa umelala sakafuni kifudifudi ukiwa na mtandio shingoni mwake.

Taarifa zinaeleza mhadhiri huyo wa Idara ya Uhandisi Kitivo cha ICT, SAUT alikuwa anaishi na msaidizi wa kazi ambaye baada ya tukio hilo kutokea ametokomea kusikojulikana.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano Novemba 30, 2022, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Buzuruga Mashariki, Martin Muya amethibitisha kutokea tukio hilo.

Amesema pamoja na kujua Hamida alikuwa anaishi na mfanyakazi wa ndani ila hakuwahi kumtambua kwa sura japo anajua alikuwa na umri kati ya miaka 15 hadi 18 kwani hakuwahi kumtambulisha ofisini kwake.

Mtoto wa mhadhiri huyo, Rehema Mbaga amesema taarifa ya uchunguzi wa mwili uliyofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando unaonyesha mama yake aliuwawa kwa kunyongwa na kitambaa shingoni.

Rehema ameileza Mwananchi Digital taarifa ya mama yake kutoonekana aliipata Jumatatu kutoka kwa mmewe ambaye alikuwa na ahadi ya kukutana naye siku hiyo bila mafanikio.


"Mme wangu alivyompigia bila mafanikio aliniambia ikabidi nimpigie jirani yake, Tatu Issa ambaye naye alifika na kugonga mlango lakini haukufunguliwa, kwa sababu ilikuwa jioni tulidhani labda ametingwa na majukumu yake ya ufundishaji tukasema tumtafute kesho yake (jana jumanne)," amesema

Amesema akiwa na mmewe, jana Jumanne waliamkia nyumbani kwa Hamida na kukuta mlango umefungwa ndipo wakaomba kibali cha kuvunja mlango wakiwa na askari wa Polisi wa kituo cha Buzuruga na kukuta mwili wa mama yake ukiwa sakafuni.

"Tulipopekua tulikuta miguu ikiwa kolidoni huku sehemu nyingine ya mwili ikiwa chumbani kama alikuwa anajibuta hivi lakini mfanyakazi wa ndani hatukumpata na kadi za benki za marehemu nazo hazionekani zilipo," alisema

"Baada ya hapo Polisi walichukua mwili na kuupeleka Bugando kwa uchunguzi zaidi ambao umeonyesha alifariki kwa kunyongwa shingoni," amesema Rehema

Taarifa ya kifo cha Hamida imethibitishwa pia na Afisa Uhusiano SAUT, Living Komu ambaye kupitia taarifa iliyosambazwa chuoni hapo ameeleza kupokea kwa masikitiko kifo cha mhadhiri huyo.

Alipopigiwa simu, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa simu yake iliita bila kupokelewa hata hivyo wakizungumza kwa sharti la kutotajwa jina mmoja wa askari wa polisi walikiri kuwa na taarifa ya mauaji ya mhadhiri huyo.

Mwili wa Hamida unatarajiwa kuzikwa kesho Alhamisi Disemba Mosi katika makabuli ya Waislamu yaliyoko Buzuruga mkoani Mwanza.

Mwananchi 


from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/CKZqYOg
via IFTTT

Comments

Popular posts from this blog

MASHAIRI MATAMU YA MAPENZI

What Happened To Sarafina Skin? From Brown To White Skin – How Did It Happen? Explore The Real Story