Serikali Yabariki Ndoa ya Bandari, TICTS Kuvunjwa



Dar es Salaam. Siku moja baada ya taarifa kuhusu nia ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kutohuisha mkataba na kampuni binafsi ya kimataifa ya kuhudumia makontena Tanzani (TICTS), Serikali imebariki uamuzi huo.

Hatua ya TPA kumalizana na TICTS iliyohudumu bandarini kwa miaka 22 imetokana na kufikia ukomo wa mkataba wa miaka mitano waliosaini Julai, 2017, pia ni kutoafikiana katika majadiliano ya kuongeza muda wa huduma.

Mkataba kati ya TPA na TICTS ulikoma Septemba 30, mwaka huu na kabla ya hatua hiyo, vilifanyika vikao kadhaa kuuhuisha bila mafanikio.

Jana, Mwananchi liliripoti kuhusu uamuzi huo wa manejimenti ya TPA, lililoupata kutoka katika chanzo cha ndani cha kuaminika kuwa TPA na TICTS walioanza kufanya kazi pamoja mwaka 2000, wanakwenda kuachana.


Kulingana na chanzo hicho, uamuzi wa TPA kuachana na TICTS unatokana na wawili hao kushindwa kuafikiana katika vigezo na masharti kama vilivyoainishwa katika ibara ndogo ya 2.2.1 ya mkataba.

“Kwa kuwa mkataba hautahuishwa moja kwa moja kama ilivyoainishwa katika ibara ndogo ya 2.2.1 ya mkataba, Menejimenti inaomba Bodi ya Wakurugenzi kupokea, kusimamia kwa makusudi na kuelekeza kadri itakavyoona sahihi.

Jana, gazeti hili lilimtafuta Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi anayeshughulikia Uchukuzi, Gabriel Migire aliyebainisha kuwa kinachotakiwa ni huduma bora ndani ya bandari.


“Hadi TPA inafikia uamuzi huo nafikiri imechukua tahadhari hiyo na mtaendelea kuona,” alisema.

Migire alieleza mkataba wa huduma ulisainiwa kati ya wawili hao na wao ndiyo wenye mamlaka ya kuusitisha, akisisitiza kinachoangaliwa na wizara ni huduma zisiathirike.

Hata hivyo, Mwananchi lilizungumza na mmoja wa maofisa kutoka TICTS, ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema ni vigumu kueleza chochote kwa sasa kwa kuwa hawajapokea taarifa rasmi.

“Taarifa hiyo tumeiona kwenye magazeti tu, mtusubiri tupate taarifa za kina kisha ndiyo tutakuwa na la kuzungumza, lakini kwa sasa mimi mwenyewe nimeona kwenye magazeti tu,” alisema.


Alipoulizwa iwapo watawasilisha ofa mpya ya kuongeza mkataba kwa mujibu wa masharti ya TPA, Ofisa huyo alikisisitiza kile inachokisimamia, hana nafasi nzuri ya kuzungumza bila taarifa rasmi.

Alitaka yatumwe maswali kwa Mtendaji Mkuu ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kuisemea kampuni hiyo, ingawa alisema hataweza kufanya hivyo hadi naye atakapopata taarifa rasmi na sio magazetini.

Hata hivyo, taarifa ambazo gazeti hili linazo kutoka ndani ya TPA zinaeleza kuwa tayari barua kwenda TICTS ikieleza nia ya kutohuisha mkataba huo imeshatumwa.

“Barua imeandikwa na bila shaka ilitumwa jana (juzi) jioni, kwa hiyo kila kitu kimepangiliwa, ikiwemo maandalizi ya kuanza kutoa huduma sisi wenyewe, wakati masuala mengine yakiendelea,” alisema.


Chanzo chetu ambacho kilisisitiza kutokutajwa jina kilisema, “Watu wasiogope kuwa huduma zitadidimia, kila kitu kimepangiliwa katika kipindi cha mpito kwani tulikuwa tunajua kila kitu, wananchi wataona na wasiwe na wasiwasi.”

Gazeti hili lilimtafuta Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mkeli Mbossa na kueleza yupo nje ya nchi na akirejea atakuwa katika nafasi nzuri ya kuzungumzia suala hilo.

Mmoja wa vigogo katika huduma za bandari (hakutaka kutajwa jina), aliueleza uamuzi huo kwa mtazamo tofauti, akisisitiza TPA na TICTS ziketi kuzungumza zaidi hadi kufikia muafaka.

Alisema hoja yake inatokana na ukweli kwamba, TICTS imekuwa na mchango mkubwa katika huduma za makontena ndani ya bandari ya Dar es Salaam.

Alikwenda mbali zaidi na kubainisha iwapo wawili hao hawataafikiana, kuna hatari ya kuyumba kwa huduma za makontena katika bandari hiyo na kusababisha msongamano.


“Hata akipatikana mwekezaji mpya kuna hatari kwamba tutapitia kwenye changamoto ya uzoefu katika huduma, tutajikuta tunakutana na msongamano,” alisema.


from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/dgD78z5
via IFTTT

Comments

Popular posts from this blog

What Happened To Sarafina Skin? From Brown To White Skin – How Did It Happen? Explore The Real Story

MASHAIRI MATAMU YA MAPENZI