Ishu ya Kocha wa Simba Roberto Oliveira, Maswali Ni Mengi Kuliko Majibu



“KOCHA Mkuu, Roberto Oliveira ameondoka usiku huu kwenda kwao Brazil kwa shughuli binafsi za kifamilia na anatarajiwa kurejea nchini mwishoni mwa mwezi huu.” Hii ni taarifa fupi ambayo ilitolewa na uongozi wa Simba kupitia vyanzo vyao rasmi vya taarifa usiku wa kuamkia jana Jumanne.

Taarifa hii ilipokelewa kwa mitazamo tofauti na wadau wengi wa soka hususan mashabiki wa Simba, wapo ambao walionekana kumtakia kila la heri kocha huyo na kumuombea safari njema ikiwemo kurudi salama.

Lakini pia wapo ambao bila kujali ni shughuli gani imempeleka kwao kocha huyo waliona kama hiyo ni ahueni kwa timu yao.

Licha ya kwamba haijawekwa wazi ni shughuli gani zilizompeleka Robertinho Brazil, lakini tayari mitandaoni kumeanza uvumi usio rasmi kuwa tayari ni makubaliano ya pande mbili na huenda kocha huyo asirudi tena.



Waswahili waliwahi kusema kuwa lisemwalo lipo na kama halipo basi linakuja, hivyo binafsi sipendi kupotezea tu taarifa hizi hewani. Tuna nafasi ya kusubiri na kuona ikiwa ni kweli kocha atarejea mwishoni mwa mwezi au la, lakini kuna usemi usemao “Samaki mkunje angali mbichi, ukisubiri akauke atavunjika.”

Hivyo wakati tunaendelea kumsubiri samaki akauke ni muhimu kuwakumbusha Simba kama kweli kuna kitu kinaendelea jii ya hili basi wana nafasi ya kurekebisha hali ya mambo.

Taarifa za ndani zinaeleza kuwa hali ya mambo bado haijakaa sawa ndani ya kikosi cha Simba, kuna mgawanyiko juu ya namna ambavyo kumekuwa na mkanganyiko wa uhusiano kati ya baadhi ya viongozi wa benchi la ufundi na baadhi ya wachezaji.
Kwa baadhi ya watu wanadhani kuna ufanano kati ya kinachoendelea sasa ndani ya Simba na kile ambacho kilitokea mwanzoni mwa msimu kwa aliyekuwa kocha wa kikosi hicho Mserbia, Zoran Maki ambaye alihudumu kwa kipindi cha siku zisizozidi 57 tu.

Zoran aliondolewa Simba kwa makubaliano ya pande mbili huku safari hiyo ikiwahusu pia aliyekuwa Kocha Msaidizi Sbai Karim na Kocha wa Makipa, Mohammed Rachid.

Ukiachana na hilo maswali yanazidi kuwa mengi pale unapokumbuka kuwa kocha wa Simba ameondoka katika kipindi ambacho timu hiyo inajiandaa na mchezo muhimu wa kusaka nafasi ya kucheza robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports dhidi ya Coastal Union.

Lakini ikumbukwe Februari 10, mwaka huu Simba ambao ni wawakilishi pekee wa Tanzania katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wanatarajia kucheza mchezo wao wa kwanza wa hatua ya makundi ya mashindano hayo.

Katika siku za hivi karibuni Simba imekuwa na rekodi tata dhidi ya waajili wao hususan makocha hali ambayo inapelekea kuwa na sintofahamu kwa mashabiki zinapotoka taarifa kama hii iliyotolewa juzi.

Kama ni kweli kuna zaidi ya kile kilichoelezwa basi nadhani ni muda uongozi wa Simba unapaswa kujifanyia tathimini ya kina kujua nini, na wapi wanataka kwenda.

Wasipokuwa makini huenda wakaenda hatua mbili na kurudi hatua kumi nyuma halafu wakaendelea kujipongeza bila kujali hatua nane walizopoteza.

Kuna kitu cha kujiuliza kuhusiana na hii timuatimua ya makocha Simba ina maana gani? Wapi kuna shida ndilo suala la kuanza nalo kwani kama watalea hili tatizo makubwa yatawakuta na watafukuza makocha kila siku.

Uchambuzi na Joel Thomas




from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/E32YUhm
via IFTTT

Comments

Popular posts from this blog

MASHAIRI MATAMU YA MAPENZI

What Happened To Sarafina Skin? From Brown To White Skin – How Did It Happen? Explore The Real Story