UBISHI WA MZE EWA KALIUA: Umemuona Clatous Chama?




HADI leo ukiniuliza kwa nini Clatous Chama yuko Tanzania siwezi kukupa jibu la moja kwa moja. Nitajikanyaga kanyanga. Nitajigonga gonga tu. Mchezaji pekee mwenye utu na utulivu. Mchezaji mwenye akili kubwa sana ya soka.

Watu wengi wanawahusudu sana wachezaji wenye mabao mengi, lakini Chama ni zaidi ya mabao. Anaufanya mpira kuonekana mchezo rahisi sana kwenye miguu yake. Unaweza kuhisi miguu yake ina sumaku. Kila mpira unapofika kwenye miguu yake unakutana na utu na utulivu.

Ni wachezaji wachache wamekuwa na baraka hii ya miguu. Hadi leo ukiniuliza ni kwa nini Chama bado anacheza soka Tanzania siwezi kuwa na jibu la moja kwa moja. Kuna mahali nitajigongagonga tu. Kuna mahali nitajikanyaga.

Chama aliwahi kusajiliwa na Klabu ya Al Ittihad Alexandria ya Misri, lakini aliondoka bila kucheza hata mechi moja rasmi. Chama amewahi kusajiliwa na RS Berkane ya Morocco, lakini aliondoka kama mchezaji aliyeshindwa. Ukitazama ufundi miguuni mwake na akili kubwa anayoitumia kwenye kufanya uamuzi, huwezi kupata majibu haraka haraka. Chama ni fundi kweli kweli. Chama anajua kuwatesa mabeki wa timu pinzani pengine kuliko mchezaji mwingine yeyote wa kizazi hiki.


Kumekuwa na hoja kuwa Chama hana nguvu na kasi. Nakubaliana kabisa na mtazamo huu, lakini sio mara zote uwanjani unahitaji watu wa kukimbia tu. Sio mara zote uwanjani unahitaji watu wa kugongana tu, muda mwingine unahitaji akili kubwa kutawala nguvu na mbio. Muda mwingine unahitaji kuwa na Chama ili kuleta utu na utulivu.

Kwanini Chama ameshindwa kucheza na kutakataka nje ya Tanzania? Siwezi kuwa na jibu la moja kwa moja. Mpira ni mchezo unaochezwa sana kichwani kuliko miguuni. Unahitaji akili kubwa kufanya uamuzi. Unahitaji akili iliyochangamka. Achana na mabao aliyofunga Chama dhidi ya Horoya kwenye mechi ya kufuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, tazama uamuzi sahihi aliokuwa anaufanya kwa wakati. Tazama utulivu wake akiwa anaelekea kwenye eneo la mwisho la kushambulia. Chama yuko kwenye dunia yake hapa

nchini. Anaweza kuamua muda wa kuwakimbiza wapinzani. Anaweza kuamua muda wa kuwatembeza. Ni kama ana ‘rimoti kontro’. Tuna bahati sana ya kupata wachezaji wa aina hii. Hadi leo ukiniuliza kwa nini ameshindwa kutamba nje ya Tanzania siwezi kuwa na jibu la moja kwa moja, kuna mahali nitajikanyaga tu.

Tofauti na watu wengi walivyofikiria, Simba imetinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kibabe sana. Chama ametinga robo fainali kibabe sana. Mabao 7-0 dhidi ya Horoya ni zaidi ya zawadi. Hat-trick safi kwa Mwamba wa Lusaka ni zawadi ya mapema zaidi kueleka Pasaka. Kama una kijana anayecheza eneo la kiungo na anamuona Chama alivyoshindwa kuleta makeke nje ya Tanzania anaweza asicheze tena mpira. Ubora wa Chama unaonekana zaidi akiwa Tanzania.

Hakucheza kabisa Misri. Hakuwa na tija kabisa pale Morocco. Ukiniuliza kwa nini? Siwezi kuwa na jibu la moja kwa moja. Kuna mahali nitajikanyaga tu. Kuna mahali nitajigongagonga.

Bado Simba haionekani kuwa bora sana, lakini inazidi kusonga mbele. Bado Simba haikupi uhakika wa safari, lakini iko tayari robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mchezo wa mpira wa miguu wakati mwingine hutupa matokeo tusiyotarajia sana. Huenda muda wa Simba kutinga nusu fainali ndiyo sasa. Muda ambao watu wachache zaidi ndiyo walioipa nafasi Simba, huenda ndiyo muda wa kuandikisha historia mpya. Kama Mwamba wa Lusaka ataendelea kuwa fiti, burudani kwa Mkapa sio ya kukosa. Kama Chama ataendelea kuwa salama, Simba pia itaendelea kuwa kwenye mikono salama.

Simba imetinga robo fainali mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika na moja ya Kombe la Shirikisho hivi karibuni, lakini hii ya safari hii ina upekee sana. Ni Simba inayoonekana kupungua ubora. Ni Simba inayoonekana kuzidiwa na Yanga. Ukitazama uchezaji wao bado haukupi uhakika wa furaha lakini ndiyo timu pekee kutoka Afrika Mashariki kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Simba wako daraja lingine kabisa Afrika. Wana dunia yao kwenye michuano hii kwa ukanda wetu. Robo fainali sio mafanikio makubwa tena kwao. Robo fainali ni kawaida tu. Wakati mwingine kwenye maisha pale unapoonekana huna ubora ndiyo muda wa kuwaziba watu midomo kwa kufanya vizuri.

Hiki ndicho Simba wanachojaribu kufanya. Hiki ndicho kinachoweza kuwapeleka Simba mbele. Watu kama Chama ni wakomavu wa mambo haya. Aina ya wachezaji ambao muda wowote wanaweza kuamua matokeo. Mashindano makubwa siku zote yanahitaji wachezaji wakubwa. Chama yuko katika mikono salama kabisa pale Msimbazi. Burudani iendelee.



from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/OCH3meV
via IFTTT

Comments

Popular posts from this blog

What Happened To Sarafina Skin? From Brown To White Skin – How Did It Happen? Explore The Real Story

MASHAIRI MATAMU YA MAPENZI