JKT yataja vigezo kwa Vijana wa nafasi za kujitolea wanaotaka kujiunga Mafunzo ya JKT 2023
Na Ezekiel Mtonyole – Dodoma
Jeshi la Kujenga Taifa JKT limewataka vijana wote kutoka Tanzania Bara na Visiwani wenye sifa za kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga taifa JKT kwa kujitolea kwa mwaka 2023 huku likibainisha kuwa vijana wenye taaluma ya Uhandisi Ujenzi, Ufugaji, Uvuvi, Saikolojia na wanyamapori watapewa kipaumbele.
JKT pia limesisitiza kuwa nafasi hizo haziuzwi na waombaji wasirubuniwe na mtu yeyote kwa kumpa fedha ili kufanikisha yeye kupata nafasi za kujiunga na JKT.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Makao Makuu ya JKT Chamwino Mkoani Dodoma Mkuu wa Tawi la Utawala Jeshi la Kujenga Taifa JKT Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema usaili utaanza Agosti 28, 2023 kupitia Mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani.
“Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa JKT Meja Jenerali Rajabu Mabele anawakaribisha vijana wote watakaopata fulsa kuja kujiunga ili kujengewa uzalendo, Umoja wa kitaifa, Ukakamavu, kufundishwa stadi za maisha na utayari wa kulijenga na kulitumikia taifa lao” amesema Brigedia Jenerali Hassan Mabena.
Amesema utaratibu wa vijana kuomba na hatimaye kuchaguliwa kujiunga na mafunzo hayo unaratibiwa na ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wilaya ambako mwombaji anatoka.
Ameongeza kuwa “ Vijana watakaochaguliwa watatakiwa kuripoti kwenye Makambi ya JKT kuanzia Septemba 26 hadi 29, 2023, aidha JKT linapenda kuwaarifu Vijana watakaopata fulsa hiyo kuwa halitoi ajira, wala kuwatafutia ajira kwenye asasi, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali au vyombo vya ulinzi na Usalama” amesema.
Aidha amebainisha kuwa muombaji mwenye elimu ya darasa la saba awe na umri wa miaka 16 hadi 18 waliomaliza elimu ya msingi kuanzia mwaka 2020, 2021, 2022 na awe na chati halisi cha kumaliza elimu ya msingi.
Vijana wenye elimu ya kidato cha nne umri usiwe zaidi ya miaka 20 waliomaliza elimu ya Sekondari kuanzia mwaka 2020, 2021, 2022 na awe na cheti halisi cha kumaliza elimu ya sekondari na cheti halisi cha matokeo na awe na ufaulu wa kuanzia daraja la kwanza hadi daraja la nne na mwenye ufaulu wa daraja la nne awe na ufaulu wa alama kuanzia 26 hadi 32.
Amesema vijana wenye elimu ya kidato cha sita umri usiwe Zaidi ya miaka 22 na awe amemaliza elimu ya Sekondari kuanzia mwaka 2020, 2021, 2022 na awe na cheti halisi cha kumaliza elimu ya sekondari , cheti halisi cha matokeo na awe na ufaulu kuanzia daraja la kwanza hadi la nne.
Kwa upande wa vijana wenye elimu ya stashahada umri usiwe zaidi ya miaka 25 awe na vyeti vya Sekondari na chuo, na vijana wenye shahada umri usiwe zaidi ya miaka 30 na awe na vyeti vya sekondari na chuo, na vijana wenye elimu ya shahada ya uzamili umri usiwe Zaidi ya miaka 30 awe na vyeti vya sekondari na cheti cha chuo.
Ameongeza kuwa “Vijana watakaochaguliwa wanatakiwa kuja na vifaa kama bukta ya rangi ya dark blue, raba za michezo zenye rangi ya kijani au blue, shuka za kulalia rangi blue bahari, soksi rangi nyeusi, nguo za kuzuiabaridi watakaopangwa kwenye mikoa yenye baridi, flana ya rangi ya kijani kibichi yenye kola ya duara isiyo na maandishi” amesema.
Sifa za muombaji na maelekezo ya vifaa wanavyotakiwa kwenda navyo vinapatikana katika tovuti ya JKT ambayo ni www.jkt.go.tz
from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/5MQ0vSJ
via IFTTT
Comments
Post a Comment