CCM yasimamisha viongozi tuhuma kukihujumu chama




CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Rukwa kimewasimamisha uongozi viongozi wa chama hicho wanaotuhumiwa kukihujumu kwa kuwauzia kadi za kielektroniki viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ili wazitumie katika mikakati yao ya kisiasa.

Akitoa taarifa hiyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Godfrey Mwanisawa, alisema viongozi hao walikuwa wakichukua kadi za wanachama na kumuuzia Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Rukwa, Sadrick Malila, maarufu kwa jina la Ikuwo ili atangaze kuwa wanachama hao wamehamia CHADEMA na wamerudisha kadi za CCM.

Alisema baadhi ya kadi hizo ni ya aliyekuwa mwana CCM mkongwe marehemu Chrisant Mzindakaya pia marehemu Zuberi Kauzeni ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi tawi la King’ombe Kata ya Majengo pamoja na kadi za wanachama waliohama mkoani Rukwa.

Alisema kuwa baadhi ya viongozi wa CCM waliokuwa wakiuza kadi hizo ni Chriss Mwalwanda ambaye ni Katibu Kata ya Majengo, Alexander Kasongo Katibu wa Siasa na Uenezi Kata ya Majengo na Paul Kawambula Katibu wa UVCCM Kata ya Majengo ambao wamesimamishwa ili kupisha uchunguzi wa tuhuma hizo.

“Oktoba 2, Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Rukwa aliita vyombo vya habari na kuonesha kadi za kielektroniki za wanachama wa CCM akidai kuwa wamerudisha na kujiunga na CHADEMA, kumbe baadhi yao walikuwa ni marehemu na wengine wamehama mkoa ambazo aliuziwa na viongozi hao wanaotuhumiwa,” alisema Mwanisawa.


Alisema, kitendo alichofanya Mwenyekiti wa Chadema si sawa kwa kuwa mwanachama anayetakiwa kurudisha kadi anapaswa akabidhi yeye mwenyewe katika ofisi ya chama anachohamia ama katika mkutano wa hadhara wa chama, lakini kilichofanyika ni siasa chafu zisizo na tija katika nyakati hizi ambazo wanachama wanauelewa mkubwa wa masuala ya kisiasa.

Pia kutokana na maendeleo makubwa yaliyofanywa na serikali ya CCM hakuna mwanachama atayerudisha kadi yake kizembe na kuwataka wanachama wa chama hicho Mkoa wa Rukwa kutulia, kushikamana na kuwa na umoja kwa kuwa CCM ipo imara na haitatetereka kwa propaganda hizo chafu.

Katibu wa CCM Wilaya ya Sumbawanga, Tabu Hussein, alisema kwa kawaida kadi za wanachama baada ya kutengeneza ngazi ya taifa zinatumwa kwa viongozi wa mkoa, nao wanazipeleka ngazi ya wilaya na huzikabidhi kwa viongozi wa kata ambao waliokuwa wakimuuzia kiongozi huyo wa Chadema.


Alisema tayari chama hicho kimeanzisha uchunguzi kwa viongozi hao wasio waadilifu pia kitachukua hatua kupitia wanasheria wa chama kwa mwanasiasa huyo wa upinzania aliyekuwa akifanya siasa chafu na kamwe CCM wilaya haitavumilia kuona wanasiasa wakiharibu nia yake nzuri ya kushinda chaguzi zijazo.


Chanzo: IPP


from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/OZnt5Ar
via IFTTT

Comments

Popular posts from this blog

What Happened To Sarafina Skin? From Brown To White Skin – How Did It Happen? Explore The Real Story

MASHAIRI MATAMU YA MAPENZI